1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Niger yaukataa ujumbe wa upatanishi wa Umoja wa Mataifa

9 Agosti 2023

Juhudi za kuutatuwa mkwamo wa kisiasa nchini Niger zinaonekana kukwama, baada ya watawala wapya kukataa kukutana na wawakilishi wa Umoja wa Mataifa na jumuiya ya ECOWAS ikielekea kuamua juu ya hatua za kijeshi.

Niger, Niamey | General Abdourahmane Tchiani bei einer Kundgebung von Anhängern der Putschisten
Picha: Balima Boureima/AA/picture alliance

Serikali ya kijeshi ya Niger iliukatalia ujumbe uliowajumuisha wawakilishi wa Umoja wa Mataifa na wa mataifa kadhaa ya Afrika siku ya Jumanne (Agosti 8).

Huo ni msimamo wa karibuni kabisa unaoongezea ugumu wa utatuzi wa mzozo huo, ambapo watawala wapya wa kijeshi wameendelea kukaidi shinikizo la kimataifa.

Soma zaidi: Blinken: Kundi la Wagner linatumia mapinduzi ya Niger kwa manufaa yake

Uamuzi huo pia ulitokea siku moja tu kabla ya mkutano wa kilele wa mataifa wanachama wa Jumuiya ya Uchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS), ambao utazungumzia uwezekano wa kutumia nguvu. 

Uamuzi huo umezima matumaini ya mwisho yaliyokuwepo ya kuupatia mzozo huo suluhisho la kidiplomasia na kuzuwa wasiwasi wa kutanuka kwa mgogoro huo kutokea taifa lenye eneo kubwa kabisa katika ukanda wa Sahel na lenye uzoefu wa matukio ya mapinduzi na uasi wa makundi ya Kiislamu..

Mali, Burkina Faso zalitaka Baraza la Usalama kuzuwia uvamizi 

Hiyo hiyo Jumanne, Mali na Burkina Faso, ambazo pia zinaongozwa na wanajeshi, zililindikia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuliomba lizuwie hatua yoyote ya kijeshi dhidi ya Niger.

Ujumbe wa wanajeshi wa Burkina Faso na Mali ukiwasili mjini Niamey kuonesha uungaji mkono wao kwa watawala wapya wa kijeshi wa Niger.Picha: RTN/Reuters

Kwenye barua hiyo, mataifa ambayo yenyewe ni wanachama wa ECOWAS walio kwenye vikwazo kwa mapinduzi ya kijeshi, yalisema "hatua kama hiyo itakuwa na matokeo mabaya na inaweza kuivunja jumuiya ya ECOWAS."z

Soma zaidi: ECOWAS bado inatumai kuna fursa ya upatanishi Niger

"Serikali za Mpito za Burkina Faso na Jamhuri ya Mali zinaliomba Baraza la Usalama kutekeleza wajibu wake wa kimsingi... kutumia njia zote lililozonazo kuzuwia hatua za kijeshi dhidi ya dola huru." Ilisema sehemu ya barua hiyo, iliyosainiwa na mawaziri wa mambo ya kigeni ya nchi zote mbili, na kusambazwa kwenye mtandao wa X.

Mawaziri hao wa mambo ya kigeni walisema wamejitolea kusaka suluhu kwa njia za kidiplomasia na majadiliano, ingawa hawakueleza undani wa juhudi hizo.

Hapo kabla, Mali na Burkina Faso zilishaapa kwamba zingeliitetea Niger endapo ECOWAS ingelijaribu kuivamia kijeshi, zikisema kwamba zinachukulia uvamizi dhidi ya Niger kuwa tangazo la vita kwao wao pia.

Marekani, ECOWAS zaendelea kushinikiza

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alisema hapo jana kwamba amezungumza na rais aliyepinduliwa, Mohamed Bazoum, aliyemuelezea juhudi zinazoendelea kupata suluhisho la amani la mzozo huu.  

Blinken alisema nchi yake inaendelea kutoa wito wa kuachiliwa haraka kwa Bazoum na familia yake.

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, Antony Blinken (kushoto), akisalimiana na Rais Mohamed Bazoum wa Niger kabla ya rais huyo kupinduliwa.Picha: Presidency of Niger/AA/picture alliance

Rais huyo aliyeingia madarakani miaka miwili iliyopita amekuwa kizuizini tangu alipopinduliwa tarehe 26 Julai.

Soma zaidi: Matumaini ya usuluhishi Niger kabla ya mkutano wa ECOWAS

Siku ya Jumanne, Rais wa Nigeria na mwenyekiti wa sasa wa jumuiya ya ECOWAS, Bola Tinubu, alitangaza vikwazo vipya hapo jana vinavyolenga mali na watu wanaohusika na mapinduzi ya Niger, huku akisema uwezekano wa hatua nyengine kubwa bado upo.

ECOWAS imesema matumizi ya nguvu itakuwa njia ya mwisho endapo wanajeshi hawataondoka madarakani na kumuachia Rais Bazoum.

Tayari wakuu wa ulinzi wa mataifa wanachama wa jumuiya hiyo wameshakubaliana juu ya mpango kazi wa kijeshi, ambao wakuu wa serikali zao wanatazamiwa kuujadili kwenye mkutano wa kilele hapo kesho mjini Abuja, Nigeria.

Vyanzo: Reuters, AP