1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wagombea wataka amani Nigeria baada ya uchaguzi kuahirishwa

Daniel Gakuba
16 Februari 2019

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari na mpinzani wake mkuu katika uchaguzi mkuu ambao umeahirishwa, Atiku Abubakar, wameelezea kusikitishwa na hatua ya kucheleweshwa kwa uchaguzi huo, lakini wote wamehimiza watulivu.

Nigeria - Wahl verschoben
Tume ya uchaguzi imetoa sababu za vifaa na kimpango kwa ucheleweshaji wa uchaguziPicha: Reuters/S. Maikatanga

Saa chache kabla ya vituo vya kura kufunguliwa, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Nigeria (INEC) Mahmood Yakubu amesema ucheleweshaji huo ulihitajika ili kuwezesha uchaguzi huru na wa haki.

''Baada ya uchunguzi makini tume imehitimisha kwamba uchaguzi hauwezi kuendelea kama ilivyokuwa imepangwa.'' amesema Yakubu, na kuongeza kuwa haukuwa uamuzi uliochukuliwa kirahisi.

Wagombea wakuu watupiana lawama

Pamoja na kuomba utulivu, wagombea hao wanaoongoza katika kinyang'anyiro cha urais wamesema wamesikitika, na kutupiana lawama.

Wagombea wakuu katika uchaguzi wa Nigeria uliocheleweshwa: Muhammadu Buhari (kushoto) na Atiku Abubakar

Festus Keyamo ambaye ni msemaji wa kambi ya Buhari, amekishutumu chama kikuu cha upinzani cha People's Democratic Party (PDP) kula na njama na tume ya uchaguzi katika kuahirishwa huku kwa uchaguzi.

''Ni matumaini yetu kwamba INEC itaendelea kutoegemea upande wowote, kwa sababu tetesi zimeenea, zikisema PDP kimekula njama na tume ya uchaguzi kuahirisha upigaji wa kura kwa sababu hakikuwa tayari.'' amesema Keyamo.

Kwa upande mwingine lakini, chama cha PDP nacho kimerudisha lawama upande wa chama cha All People's Congress (APC) cha Muhammadu Buhari, kikidai kucheleweshwa kwa uchaguzi ni mbinu ya kiongozi huyo kuendelea kung'ang'ania madarakani.

''Hii ni hatua ya hatari sana kwa demokrasia yetu, na haikubaliki.'' amesema msemaji wa chama cha PDP, Uchoe Secondu.

Wapiga kura wavunjika moyo

Wapiga kura katika majimbo yote ya Nigeria ambao wengi walikuwa wamesafiri kwenda katika majimbo yao, wamelaani ucheleweshwaji wa zoezi la uchaguzi.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi Nigeria, Mahmood YakubuPicha: Getty Images/AFP/K. Sulaimon

Auwolu Usman kutoka mji wa Maiduguri amelalamika, ''Usiku mzima hatukupata usingizi, tukiwa na matumaini ya kupiga kura asubuhi ya leo, lakini tumeishia kuambiwa uchaguzi umeahirishwa.''

Kulingana na sheria ya uchaguzi ya Nigeria, mtu sharti apige kura katika jimbo analotoka.

Rais Muhammadu Buhari ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 2015, anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa Atiku Abubakar, mfanyabiashara tajiri ambaye aliwahi pia kuwa makamu wa rais.

Wote wawili walikuwa wamesafiri kurudi katika majimbo yao kaskazini mwa nchi, Buhari katika jimbo la Katsina na Abubakar nyumbani kwake Adamawa, ambako walitarajiwa kupigia kura. Wasaidizi wao wamesema wote wawili watarejea haraka katika mji mkuu, Abuja.

Boko Haram yashambulia

Huku macho na masikio ya watu vikiwa vimeelekezwa katika taarifa hizo za kucheleweshwa kwa uchaguzi, kundi la waasi wa kijihadi, Boko Haram limeripotiwa kuuwa watu 8 katika jimbo la Maiduguri, Kaskazini Magharibi mwa Nigeria.

Shambulizi hilo limethibitishwa na Haram Abba Aji-Kalli, kutoka kundi la wanamgambo wa kiraia, aliyezungumza na shirika la habari la AFP.

Mwandishi: Daniel Gakuba/rtre, afpe,

Mhariri: Sylvia Mwehozi