Nigeria: Mripuko waua watu 50 msikitini
22 Novemba 2017Kiasi cha watu 50 wameuawa wakati mvulana mmoja alipojiripua ndani ya msikiti kaskazini mashariki mwa Nigeria katika shambulizi linalohusishwana kundi la Boko Haram.
Shambulizi hilo lilitokea wakati wa sala ya asubuhi katika msikiti wa Madina ulioko katika mji wa Mubi, umbali wa kilomita 200 kutoka mji mkuu wa jimbo la Adamawa, Yola. Shambulizi hilo la Jumanne ni kubwa katika jimbo hilo tangu Desemba mwaka jana wakati wanawake wawili walipojitoa muhanga na kuwaua watu 45 katika soko lililokuwa na watu wengi kwenye mji wa Madagali.
Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria, ambaye karibu miaka miwili iliyopita alitangaza kundi hilo la Boko Haram limesambaratishwa kiufundi, amesema shambulizi hilo ni la kikatili.
Wachambuzi wa masuala ya usalama wanasema shambulizi hili linaashiria kitisho kinachoendelea kusababishwa na kundi hilo lenye mafungamano na kundi linalojiita Dola la Kiislamu, licha ya kupunguwa kwa idadi ya vifo vinavyosababishwa na kundi hilo katika kipindi cha mwaka jana.