Nigeria na Algeria kuibeba Afrika
30 Juni 2014Nigeria itaikabili Ufaransa katika mchezo wa kwanza na kisha baadae Algeria itaivaa Ujerumani katika uwanja wa Beira uliopo Porto Alegre.
Baada ya wapenzi wa kandanda duniani kote kushuhudia Brazil, Colombia, Uholanzi na Costa Rica zikifuzu kucheza hatua ya robo fainali ya kombe la dunia, hii leo shughuli itakuwa pevu pale Nigeria ama Super Eagles itakapokuwa inavaana na mabingwa wa kombe hilo wa mwaka 1998 Ufaransa katika mchezo utakaochezwa katika dimba la Nacional huko Brasilia.
Wakati Ufaransa itakuwa inashuka uwanjani ikiwa na nia ya kulipiza kisasi cha kufungwa na Nigeria goli 1-0 katika mchezo wa kirafiki uliochezwa mwaka 2009, Nigeria itakuwa inataka kutinga hatua ya robo fainali kwa mara ya kwanza baada ya kushindwa kufanya hivyo katika fainali za mwaka 1994 na 1998.
Kama hiyo haitoshi Super Eagles watakuwa pia wanataka kuwapa raha mashabiki wa soka wa bara la Afrika pamoja na raia wa Nigeria kwa ujumla ambao wamekuwa wakikumbwa na matukio ya milipuko ya mabomu inayosababisha watu wasiokuwa na hatia kupoteza maisha.
Kiungo mkabaji wa Nigeria, Mikel Obi amesema anaamini kuendelea kufanya vizuri kwa timu yake kutaweza kuleta umoja kwa raia wa nchi hiyo. Kocha mkuu wa Ufaransa Didier Deschamps amesema amewaambia wachezaji wake waelekeze akili zao katika mchezo dhidi ya Nigeria na wala wasifikirie hatua inayofuata kabla hawajavaana na tai hao wa Afrika magharibi.
Ufaransa inaweza ikamkosa mlinzi wake mahiri wa kati Mamadou Sakho ambaye anasumbuliwa na maumivu huku Nigeria inaweza ikamtumia winga wake machachari Victor Moses na mlinzi wa kati Godfrey Oboabona.
Baada ya mchezo huo, Algeria itavaana na Ujerumani katika mchezo mwingine wa hatua ya 16 bora ya michuano hiyo. Algeria iliyoingia kwa mara ya kwanza katika hatua hiyo ya 16 bora itakuwa inataka kuendeleza ubabe wake kwa Ujerumani ambayo ilikubali kichapo katika michezo miwili iliyowahi kukutana na mbweha hao wa jangwa.
Kocha wa Algeria Vahid Halilhodzic amesema ushindi mwaka 1982 utachangia kuwapa nguvu na ujasiri wachezaji wake katika mchezo wa leo huku Joechim Loew akisema kuwa mchezo huo hauna maana yoyote kwa wachezaji wa sasa kwakua wengi wao walikuwa hawajazaliwa.
Washindi katika michezo ya leo, watakutana katika hatua ya robo fainali ya kombe la dunia ambayo itaanza kuchezwa tarehe 4 ya mwezi huu.
Mwandishi: Anuary Mkama/afpe
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman