Kitandawili cha Boko Haram kimezungumziwa
11 Machi 2016Tuanzie lakini Nigeria ambako kesi dhidi ya rushwa inawekewa matumaini ya kufichua siri kwa nini jeshi la nchi hiyo linaonekana kuwa dhaifu mbele ya Boko Haram. Ripota wa gazeti la mjini Berlin,die Tageszeitung anaamini kitanzi kimeanza kumbana Alex Badeh. Kiongozi huyo wa zamani wa vikosi vya wanajeshi vya Nigeria atabidi ajieleze mahakamani alkhamisi inayokuja. Anatuhumiwa kutumia vibaya Euro milioni 18. Fedha hizo zililengwa kugharimia mapambano dhidi ya wanamgambo wa itikadi kali wa Boko Haram. Lakini badala ya kununua silaha na vipuri kwaajili ya vikosi vya nchi hiyo,mwendesha mashtaka anasema Badeh ametuma angalao sehemu ya fedha hizo katika akaonti ya benki ya kampuni moja inaayojenga kituo kikuu cha biashara katika mji mkuu wa Nigeria-Abuja.
Vituo kama hivyo vya kibiashara vimejaa kila pembe mjini Abuja,lengo likiwa sio tu kuwavutia watu wa tabaka ya kati wanaozidi kuongezeka,bali pia kufanya biashara ya kusafisha fedha zinazopatikana kwa njia haramu. Tume inayopambana na rushwa EFCC inamtuhumu Badeh pia kuwekeza katika jumba moja la anasa. Die Tageszeitung linasema kamatakamata iliyoanza tangu miezi michache iliyopita dhidi ya watuhumiwa wa rushwa inampandishia hadhi yake rais Muhammadu Buhari aliyechaguliwa takriban mwaka mmoja uliopita. Badeh anashikiliwa jela na anakanusha tuhuma dhidi yake. Lakini pindi zikithibitika,basi zitapata nguvu dhana za muda mrefu kwamba fedha zinazotolewa kupambana na magaidi hazijulikani zinakwenda wapi. Linamaliza kuandika die Tageszeitung.
Ndege za Marekani zawahujumu wanamgambo wa Al Shabab nchini Somalia
Hujuma dhidi ya vituo vya magaidi wa Al Shabab nazo pia zimegonga vichwa vya habari vya magazeti ya Ujerumani wiki hii. Lilikuwa gazeti la Berliner Zeitung lililoandika ripoti iliyokuwa na kichwa cha maneno "Ndege za kijeshi na zile zisizokuwa na rubani Somalia". Berliner Zeitung linaandika tunanukuu "Marekani yawauwa wanamgambo 150 wa Al Shabab. Walikuwa wakiandaa mashambulio ya kigaidi."Lilikuwa mojawapo ya mashambulio makali kabisa kuwahi kuongozwa na vikosi vya marekani nchini Somalia,linaendelea kuandika gazeti la Berliner Zeitung. Ndege za kivita sawa na zile zisizokuwa na rubani zilishiriki katika mashambulio hayo yaliyotokea mwishoni mwa wiki,na kuhujumu kambi ya mazoezi ya kijeshi ya "Raso" umbali wa kilomita 200 kaskazini mwa mji mkuu Mogadishu.
Vikosi vya Marekani vimekuwa kwa muda mrefu vikiipeleleza kambi hiyo-msemaji wa wizara ya ulinzi ya Marekani- Pentagon-Jeff Davis amenukuliwa na Berliner Zeitung akisema. Haijulikani lakini kama viongozi wa Al Shabab ni miongoni mwa waliouwawa au la. Hilo lilikuwa shambulio la pili kubwa la vikosi vya Marekani dhidi ya wafuasi wa itikadi kali wa dini ya kiislam mwaka huu linamaliza kuandika gazeti la Berliner Zeitung linalokumbusha hujuma kama hizo za mwezi uliopita wa february dhidi ya kambi za mazoezi ya kijeshi za wanamgambo wa dola la kiislam IS katika mji wa Sabratha nchini Libya ambapo magaidi 49,ikiwa ni pamoja na kiongozi wao Noureddine Chouchane waliuliwa.
Uturuki yajijenga Afrika
Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu juhudi za Uturuki za kulinyemelea bara la Afrika."Anafuata nyayo za Gaddafi" ndio kichwa cha maneno cha ripoti ya Frankfurter Allgemeine kuhusu ziara ya pili katika kipindi cha miezi 16 ya rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan barani Afrika. Baada ya ziara aliyoifanya mwaka jana katika nchi za pembe ya Afrika,safari hii ilikuwa zamu ya Afrika Magharibi ambako rais wa Uturuki alizitembelea Côte d'Ivoire,Ghana ,Nigeria na Guinea.
Frankfurter Allgemeiner linazungumzia umuhimu wa kiuchumi wa nchi hizo 4 kwa Uturuki.Wawekezaji wa Uturuki wameenea kila pembe ya Afrika. Frankfurter Allgemeiner linatoa picha ya umuhimu wa Afrika kwa Uturuki;vitega uchumi vya moja kwa moja vya Uturuki kwa Afrika vimefikia dala bilioni 23.4 mwaka jana,na kuipita Brazil iliyowekeza katika kipindi hicho hicho dala bilioni 20. Juhudi za kuimarishwa uhusiano wa kiuchumi zinakwenda sambamba na zile za kuimarisha uhusiano wa kisiasa kati ya Afrika na Uturuki,linamaliza kuandika Frankfurter Allgemeine.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/PRESSER/ALL/PRESSE
Mhariri: Gakuba Daniel