Nigeria yafufua matumaini yake kombe la dunia
23 Juni 2018Kipigo ilichopata Iceland dhidi ya Nigeria, Iceland ikiwa imefika kwa mara ya kwanza katika fainali za kombe la dunia, hakikuzika ndoto yao bado, wakati Argentina inayoyumba yumba inaweza pia kujinasua katika dakika za mwisho na kuingia katika awamu ya mtoano.
Lakini ushindi wa jana Ijumaa, kusini mwa Urusi, unashuhudia Nigeria ikiwa katika udhibiti wa majaaliwa yake wakati watakapokutana na Argentina katika mchezo wao wa mwisho wa kundi D siku ya Jumanne.
Hata hivyo Argentina inalazimika kuishinda Nigeria na kuomba Iceland isishinde dhidi ya Croatia, kwa kuwa hilo linaweza kuwapeleka Wamarekani kusini hao nyumbani na mapema, ikitegemea tofauti ya magoli.
Brazil ilihitaji jana mabao mawili katika dakika za majeruhi kuishinda Costa Rica jana wakati Philippe Coutinho na Neymar walipopachika mabao na kuwaweka washindi mara tano wa kombe hilo katika njia kuelekea timu 16 zitakazopambana katika awamu ya mtoano.
Wabrazil walionekana kuelekea katika sare yao ya pili mfululizo yenye kufadhaisha kabla ya mshambuliaji wa Barcelona Coutinho kuuweka mpira wavuni kwa kupitia katikati ya miguu ya mlinda mlango wa Costa Rica Keylor Navas katika dakika ya 91 mjini St. Petersberg.
Neymar anyimwa penalti
Neymar, ambaye alikataliwa kupewa mkwaju wa penalti na mwamuzi Bjorn Kuipers baada ya kuwasiliana na wasaidizi wa mwamuzi wanaohusika na kuangalia vidio za mchezo huo , alifunga bao la pili dakika saba katika dakika za nyongeza. Lilikuwa bao la hivi karibuni kabisa katika historia ya kombe la dunia.
Ari ya Uswisi ya kutokubali kushindwa na nia ya kutaka kushinda ilikuwa funguo ya kubadilisha matokeo katika mchezo ambao walisumbuliwa na Serbia kwa kipindi kirefu cha kwanza, kocha wa Uswisi Vladimir Petkovic alisema baada ya mchezo huo ambao Uswisi ilishinda kwa mabao 2-1.
Mchezo ulikuwa katika kasi kubwa , ambapo Serbia ilidhibiti mchezo katika kipindi cha kwanza , lakini Uswisi ilianza kwa kasi kipindi cha pili na kuiweka Serbia katika wakati mgumu.
Ujerumani inarejea dimbani tena leo ikipambana na Sweden katika pambano ambalo Wajerumani wanawania kurejesha matumaini yao ya kuendelea mbele katika fainali hizi baada ya kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Mexico katika mchezo wao wa ufunguzi katika kundi F.
Ujerumani haitakuwa katika nafasi nzuri iwapo itatoka sare na Sweden ambayo iliishinda Korea kusini katika mchezo wa kwanza. Korea kusini pia itakuwa na kibarua kigumu kuigaragaza Mexico ambayo nayo pia ina pointi 3 baada ya kuilaza Ujerumani kwa bao 1-0 katika mchezo wa kwanza.
Mchezo wa kwanza hata hivyo leo ni kati ya Ubelgiji na Tunisia, ambayo ilifanya kazi kubwa katika mchezo wake wa kwanza dhidi ya Uingereza lakini ikakubali kipigo cha mabao 2-1 katika kundi E.
Tunisia inataka kuendelea kubakia katika mashindano haya lakini ina mlima mkubwa wa kupanda kabl ya kutimiza ndoto yao hiyo hii leo dhidi ya Ubelgiji ambayo iliirarua Panama kwa mabao 3-0 katika mchezo wa kwanza.
Mwandishi: Sekione Kitojo
Mhariri: Mohammed Khelef