1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nigeria yafungiwa miaka 2 kucheza dimba kimataifa.

1 Julai 2010

Je, hilo ni dimba kati ya marais na FIFA ?

Nigeria yafungiwa kucheza miaka 2.Picha: AP

Masaa 24 kabla Black Stars-Ghana, na Uruguay na Brazil na Holland kuingia uwanjani kuamua ni timu gani 4 zitakata tiketi za nusu-finali ya kombe la Dunia na mwishoe , fainali Julai 11, kuna fainali maalumu inayochezwa sasa na marais na wanasiasa:Walioanza dimba hil, ni viongozi wa kiafrika kati yao na timu zao za Taifa:

Marehemu Rais Ahmed Sekutoure wa Guinea, Rais Yakubu Gowon wa Nigeria,Maboutu Seseko wa Zaire sasa DRC, Jenerali Achiempong wa Ghana, na sasa Goodluck Jonathan wa Nigeria , wote wamekuwa na tabia ya mchezo wa-kuingilia timu zao za Taifa.

Baada ya Rais Nicholas Sarkozy, wa Ufaransa, wiki iliopita kumwita nahodha wa Thiery Henry, Ikulu Elysee Palace kwa kikao maalumu,mbunge wa Uingereza wa chama-tawala cha Conservative,David Amess, ameitisha jana ufanywe uchunguzi maalumu na wa haraka, kuhusu msiba ulioipata England katika kombe la dunia hadi kuchezeshwa kindumbwe-ndumbwe na Ujerumani na kuzabwa mabao 4:1 pamoja na kutolewa duru ya pili.

Pasi ya rais Sarkozy , aliipokea kwanza rais Goodluck Jonathan wa Nigeria ambae jana alikisimamisha kikosi kizima cha Super Eagles,timu ya Taifa ya Nigeria, kucheza dimba la kimataifa kwa miaka 2-hata Kombe la Afrika.Kisa ? Ni jinsi Nigeria, ilivyoliabisha Taifa huko Afrika Kusini.Nigeria, ilipigwa kumbo duru ya kwanza tu.

Uamuzi wa rais Jonathan, ulikatwa siku 1 baada ya Kamati-tendaji ya Shirikisho la dimba la Nigeria (NFF), kukutana na kukagua jinsi Nigeria, ilivyotimuliwa duru ya kwanza tu na kuondokea na pointi 1 ikimaliza mkiani mwa kundi lake.

Mshauri wa mawasiliano wa rais wa Nigeria, Ima Niboro, akaarifu kwamba, waziri wa spoti wa Nigeria ,ataiandikia FIFA karibuni, kueleza msimamo iliouchukua Nigeria, juu ya Timu ya Taifa. Waziri huyo pia ametakiwa kujenga Jumba maalumu la dimba kwa Nigeria na kwamba, tatizo la timu ya Taifa ni la muundo wa dimba.

FIFA, tayari iliionya majuzi Ufaransa, kuwa serikali isicheze dimba pale rais Sarkozy, alipomuita Henry Ikulu na baadae, viongozi wa juu wa chama cha mpira kujiuzulu. Rais wa FIFA Sepp Blatter, alitishia juzi kuipiga marufuku timu ya Taifa ya Ufaransa na klabu zake zisicheze mashindano ya kimataifa ikiwa wanasiasa wa Ufaransa, hawataacha kuingilia dimba.Inavyobainika, FIFA ina finali maalumu sasa kucheza pia na Nigeria na nani atashinda -tusubiri kuona.

Uamuzi wa Rais Goodluck Jonathan, si mpya kwa Nigeria:Kumbuka, pale Nigerian "Green Eagles" kama walivyoitwa zamani-washindi wa Taji la dimba la michezo ya bara la Afrika,Lagos, 1973, walipoaibishwa muda mfupi tu baadae na Zambia,jinsi aibu ilivyokuwa kubwa,Rais Yakubu Gowon, aliivunja timu nzima ya Taifa na kuamrisha kama sasa kujengwa upya.

halafu Green eagles ilipocheza tena vibaya katika Kombe la XI la Afrika mjini Accra,Ghana ,1978, waziri wa michezo Henry Adefope alikuwa na kikao maalumu chumbani uwanjani na kuwafokea kwa kumaliza 3 na sio na kombe.Katika kombe lililofuatia,salamu za Jamadari Adefope ziliwasili na Green Eagles wakatawazwa mabingwa nyumbani lagos,1980.

Kwahivyo, Rais Goodluck Jonathan, anafuata nyayo ndefu na amewatupia sasa pasi marais na wanasiasa wa ulaya kucheza dimba.

Mwandishi: Ramadhan Ali/RTRE

Mhariri:Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW