1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nigeria yasherehekea miaka 60 tangu ilipojipatia uhuru

Sylvia Mwehozi
1 Oktoba 2020

Nigeria inasherehekea miaka 60 tangu ijipatie uhuru. Hata hivyo wengi wanasema hakuna mengi ya kufurahia kutokana na changamoto za kupanda kwa bei ya mafuta, rushwa iliyokithiri na kukosekana kwa usalama. 

Nigeria Democracy Day 2019
Picha: Reuters/A. Sotunde

Nigeria inasherehekea miaka 60 tangu ijipatie uhuru. Hata hivyo wengi wanasema hakuna mengi ya kufurahia kutokana na changamoto kadhaa zinazolikabili taifa hilo la Afrika Magharibi ikiwemo kupanda kwa bei ya mafuta, rushwa iliyokithiri na kukosekana kwa usalama. 

Bei ya mafuta katika taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa mafuta ilipanda kwa miezi mitatu mfululizo baada ya serikali kuondoa ruzuku ya nishati hiyo kwasababu ya mgogoro wa bajeti. Na sio bei ya mafuta tu ambayo imepanda, pia gharama za umeme zimeongezeka mara mbili. Bei za bidhaa za msingi kama vile mchele, maharage na unga nazo zimepanda juu tangu serikali ilipofunga mipaka yake mwaka jana kwa ajili ya kukabiliana na ulanguzi.

Mapema mwaka huu, serikali iliondoa ruzuku ya mafuta ikisema kwamba imeshindwa kuendelea kulipa kiasi cha dola bilioni 2.6 kama gharama za mafuta katikati mwa janga la ulimwengu la virusi vya corona. Mafuta ghafi yamechangia karibu theluthi mbili ya mapato ya serikali kwa zaidi ya muongo, kulingana na takwimu za Bloomberg. Kuporomoka kwa bei ya mafuta mwaka huu kumepora sehemu kubwa ya bajeti ya Nigeria.

Moja ya kiwanda cha mafuta mjini Kaduna NigeriaPicha: Construction Photography/Photoshot/picture alliance

Nigeria haiwezi kutumia rasilimali yake ya mafuta

Licha ya kuwa taifa linaloongoza afrika katika uzalishaji wa mafuta ghafi, Nigeria haiwezi kuzalisha bidhaa zitokanazo na petroli ambazo wananchi wake wanazihitaji katika maisha ya kila siku. Taifa hilo la afrika magharibi linalo viwanda vitano ambako mafuta yanageuzwa katika bidhaa nyingine kama dizeli na petroli. Kushindwa kusafisha mafuta yake yenyewe, kumeifanya Nigeria kutegemea uagizaji wa mafuta wa gharama kubwa. Soma Nigeria: Miaka 50 baada ya vita ya Biafra

Miaka 16 iliyopita rais wa wakati huo Olusegun Obasanjo alisema kwamba serikali itabadili uchumi wake mbali na mafuta na madini ili kuongeza usalama wa uchumi na kutengeneza ajira. Serikali ya rais Muhammadu Buhari ilitoa ahadi kama hizo. Ignatius Chukwa ni mwandishi wa habari za biashara anatoa mtizamo wake, akisema kuwa; 

"Utawala wa Buhari uliingia mara moja na mawazo ya kubadilisha uchumi, kitu cha kwanza kilichotokea tuliingia katika mdororo wa uchumi, kwahiyo walipambana na hali hiyo kwa miaka miwili na wakati wanataka kuinuka tena wakitumai kuwa watapanda tena mwaka huu, lililojitokeza ni ulimwengu kuanguka kutokana na janga la virusi vya corona na sekta ya mafuta ndio mwathirika mkubwa"

Ukiacha kushindwa kutumia ipasavyo rasilimali zake, Nigeria inakabiliwa vitendo vya ufisadi mkubwa. Kulingana na ripoti ya wakfu wa Konrad Adenauer, "rushwa inaenea katika kila ngazi ya jamii kutoka kwa wanasiasa wa ngazi ya juu na watumishi wa umma, maafisa wa usalama, wafanyabiashara na wanachi maskini wa taifa hilo."

Suala la kukosekana usalama nalo limeliweka taifa hilo katika wakati mgumu. Eneo la kaskazini mwa nchi limeshuhudia vitendo vya kigaidi na mashambulizi ya wanamgambo kwa zaidi ya muongo. Zaidi ya watu milioni mbili wamekuwa wakimbizi wa ndani.

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW