1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nigeria yashutumiwa kuuwa Boko Haram kikatili

Elizabeth Shoo5 Agosti 2014

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesema kuwa jeshi la Nigeria limehusika katika matukio ya kikatili kwenye mapambano dhidi ya wapiganaji wa kundi la Boko Haram.

Wanajeshi wa Nigeria
Picha: REUTERS

Shirika la Amnesty International limekusanya video na picha zinazoonyesha ukatili unaosemekana kufanyika na askari wa Nigeria. Picha hizo zinaonyesha wanajeshi wanavyowachinja wale wanaodhaniwa kuwa magaidi wa kundi la Boko Haram na kisha kuwatupa kwenye kaburi la halaiki. Amnesty International imesema kuwa imezungumza na watu walioshuhudia matukio hayo na hivyo imeweza kuthibitisha uhalisi wa picha na vidio hizo.

Akizungumza na DW, Makmid Kamara wa Amnesty International amesema, "Tumehakikisha taarifa zote tulizopewa na mashahidi. Tumezungumza na afisa wa jeshi la Nigeria ambaye hakutaka kutaja jina lake. Amethibitisha kuwa watu wanaoonekana kwenye vidio ya mauaji ni wanajeshi wa Nigeria na ametutajia hata kikosi wanachotoka."

Amnesty International imezungumza na watu wanaoeleza kushuhudia ukatili unaofanywa na wanajeshi katika matukio mengine pia. Mwaka uliopita, askari waliwapiga na kuwakata kwa mapanga wanaume wapatao 35. Polisi iliwashutumu wanaume hao kuwa wafuasi wa kundi la Boko Haram. Siku chache baadaye watu hao waliuwawa kwa risasi.

Wanigeria wataka ulinzi zaidi

Jeshi la Nigeria limekanusha mashtaka yote na kusisitiza kwamba vyombo vya ulinzi vinafuata sheria na kuheshimu haki za binadamu. Msemaji mmoja wa jeshi hata hivyo amesisitiza kuwa upelelezi wa vitendo hivyo vya kikatili utafanyika na iwapo itabainika kuwa kweli askari waliwauwa watu wanaosadikiwa kujiunga na Boko Haram, basi watafunguliwa mashtaka.

Mlipuko wa bomu la gari uliotokea mjini Maiduguri, NigeriaPicha: picture-alliance/AP Photo

Makmid Kamara wa Amnesty International anakosoa kuwa ingawa serikali ya Nigeria imetangaza hali ya hatari katika eneo la Kaskazini Mashariki ambapo uhalifu huo umefanyika, haki za binadamu bado zinakiukwa. "Haki ya kuishi bado haiheshimiwi na hatujaona kuwa hali ya usalama imeboreshwa eneo la Kaskazini Mashariki. Tunachoshuhudia ni kuongezeka kwa matumizi ya nguvu miongoni mwa wapiganaji wa Boko Haram na pia ukiukwaji wa haki za binadamu kupitia jeshi la Nigeria."

Raia wengi wa Nigeria wanaikosoa serikali yao kwa kushindwa kupambana na waasi wa Boko Haram na kuleta amani eneo la Kaskazini Mashariki mwa nchi. Hadi sasa raia wapatao 4,000 wameuliwa na kundi hilo. Mbali na hayo, wasichana zaidi ya 200 waliotekwa wakiwa shuleni bado hawajaokolewa.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/afp/dpa

Mhariri: Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW