1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nigeria yataka mitandao ya kijamii iwe na leseni za ndani

Angela Mdungu
10 Juni 2021

Waziri wa habari na utamaduni wa Nigeria, Lai Mohammed amesema makampuni ya mitandao ya kijamii yanayotaka kufanya kazi nchini humo ni lazima yajisajili na kupewa leseni.

Muhammadu Buhari, Präsident von Nigeria
Picha: Siphiwe Sibeko/REUTERS

Kauli hiyo imetolewa ikiwa ni hatua ya hivi karibuni zaidi kuchukuliwa tangu serikali ya Nigeria ilipoupiga marufuku mtandao wa kijamii wa Twitter nchini humo wiki iliyopita.

Akifafanua kuhusu uamuzi huo waziri huyo wa habari na utamaduni wa nchi hiyo alisema, "Tunasisitiza kuwa ili kuendesha shughuli Nigeria kwanza unapaswa kuwa kampuni ya Nigeria na upate leseni kutoka kwa tume ya utangazaji." Waziri Mohammed bila ufafanuzi zaidi alisema kwamba, taratibu  mpya za uendeshaji wa makampuni hayo ya mitandao ya kijamii ni pamoja na masharti ya kuendelea kuendesha shughuli.

Utaratibu huo mpya umetangazwa katikati ya kile wanachokisema wakosoaji kuwa hatua kali zinazoendelea za kuuminya uhuru wa kujieleza katika taifa hilo lenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika, jambo ambalo limesababisha lilinganishwe na enzi za utawala wa kijeshi nchini humo uliodumu kwa miongo kadhaa katika karne ya 20.

Waziri wa habari Lai Mohammed hakutaja tarehe ya mwisho ya usajili na kupata leseni kwa makampuni hayo lakini alisema kuwa baadhi ya makampuni yalishapewa notisi. Hata hivyo, hakuweka bayana  majina ya makampuni hayo na hakupokea simu wala ujumbe wa ufafanuzi kuhusu hilo.

Wiki iliyopita, Nigeria ilisitisha shughuli za mtandao wa kijamii wa Twitter nchini humo, siku mbili baada ya jukwaa hilo kuondoa chapisho la Rais Muhammadu Buhari lililotishia kuwaadhibu wanaotaka kujitenga. Katika chapisho lake hilo Rais Buhari alitolea mfano vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini humo iliyodumu kwa miaka kadhaa iliyopita katika karne ya 20, ambapo mamilioni ya raia walikufa huku akiwaonya wanaohusika na machafuko ya hivi sasa kusini mashariki mwa nchi hiyo ambako misuguano ya wanaotaka kujitenga imepamba moto.

Mkurugenzi mtendaji wa Twitter alalamikiwa

Serikali ya Nigeria ililalamika kuwa Twitter haikufuta maoni ya kuvuruga amani yaliyoandikwa na kiongozi wa wanaotaka kujitenga kutoka eneo la kusini mashariki mwa nchi hiyo. Serikali ya taifa hilo ilimtolea pia mfano mkurugenzi mtendaji wa Twitter Jack Dorsey aliyeunga mkono maandamano dhidi ya ukatili wa polisi nchini humo mwaka uliopita.

Waziri wa habari wa Nigeria, Lai MohammedPicha: DW/T. Sakzewski

"Twitter imekuwa iikiwapa jukwaa wale wanaotishia uwepo wa Nigeria," alisema Mohammed, akimtaja kiongozi wa watu wanaotaka kujitenga pamoja na waandamanaji wanaopinga ukatili wa polisi. Waziri huyo aliongeza kuwa, mitandao ya kijamii ya Facebook, Instagram na Whatsapp haijazuiwa nchini humo, lakini hakusema ikiwa itahitaji kujisajili na kupata leseni. 

Kuhusu kuruhusiwa tena kufanya kazi kwa Twitter, waziri Mohammed amesema mtandao huo wa kijamii utaruhusiwa kufanya tena shughuli zake nchini humo ikiwa nao utajisajili na kupata leseni ya kufanya kazi nchini humo na kufuata masharti.

Kuhusu lawama za kuminya uhuru wa habari Waziri wa habari na utamaduni Lai Mohammed alisema,"Hakuna mtu anayeweza kuituhumu Nigeria  kuwa inakandamiza uhuru wa kujieleza lakini kuna mipaka ambayo mtu hapaswi kuivuka"  Alisema.   

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW