Nigeria yatangaza kikosi kushiriki Kombe la Mataifa Afrika
2 Oktoba 2018Kocha wa Kandanda wa timu ya taifa ya Nigeria Gernot Rohr, ametangaza kikosi chake kwa ajili ya pambano lijalo la mashindano ya kombe la mataifa ya Afrika, dhidi ya Libya. Lakini kwa mara nyengine tena nahodha wa timu hiyo John Obi Mikel, hayumo katika kikosi hicho.
Mchezaji huyo wa zamani wa kiungo wa kilabu ya Chelsea ya Uingereza na ambaye sasa anachezea kilabu ya Tianjin ya China, alilikosa pambano la mwezi uliopita dhidi ya Seychelles, kwa sababu alikuwa ndiyo kwanza ameanza tena mazoezi baada ya kuumia.
Mlinzi wa Udinese ya Italia William Troost Ekong na Moses Simon ambao pia waliukosa mchezo na Seychelles kwa sababu ya majeraha na hali kadhlika Alex Iwobi anayechezea kilabu ya Arsenal ambaye alikuwa mgonjwa, wamerudi katika kikosi hicho.
Mchuano wa kwanza dhidi ya Libya utachezwa katika mji wa kusini mashariki wa Uyo Jumamosi ijayo na mchezo wa marudiano utafanyika Tunisia Oktoba 16, kwa sababu ya ukosefu wa usalama nchini Libya.