1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kura zahesabiwa Nigeria baada ya uchaguzi wa bunge

19 Machi 2023

Zoezi la kuhesabu kura linaendelea nchini Nigeria baada ya kufanyika uchaguzi wa kuwachagua wabunge.

Nigeria | Auszählung Wahlen
Picha: Sunday Alamba/AP Photo/picture alliance

Uchaguzi huo umefanyika wiki tatu baada ya chama tawala nchini humo kushinda uchaguzi wa urais ambao unapingwa na upinzani unaodai kuwa uchaguzi huo ulikumbwa na udanganyifu.

Rais mteule wa Nigeria Bola Ahmed Tinubu.Picha: APTN

Vyama vyote viwili vya Labour Party (LP) na Peoples Democratic Party (PDP) vimeupinga ushindi wa chama cha All Progressives Congress (APC), vikidai kuwa hitilafu za kiufundi zilitoa nafasi ya kufanyika ubabaifu kwenye kuhesabu kura lakini tume ya uchaguzi imekanusha madai hayo.

Nigeria taifa lenye watu wengi zaidi barani Afrika linawachagua zaidi ya wabunge 900 wa mabunge ya majimbo na magavana 28, kwenye uchaguzi uliokuwa na ushindani mkubwa hasa katika mji mkuu wa kibiashara wa Lagos.

Soma: Wanigeria waandamana kupinga matokeo ya uchaguzi

Kutokana na vurumai, upigaji kura uliahirishwa katika baadhi ya maeneo katika wilaya ya Eti Osa ya Lagos na katika wilaya za Asari-Toru na Degema za Jimbo la Rivers ambapo uchaguzi  umepangwa kufanyika Jumapili.

Maeneo mengine yaliyokuwa na ushindani mkali katika uchaguzi huo ni ya Rivers kusini mwa Nigeria na eneo la Kano la kaskazini. Katika eneo la Adamawa la kaskazini mashariki mwanamke wa kwanza ameibuka kuwa mshindi kwa kuchaguliwa kuwa gavana wa jimbo hilo.

Ripoti zinaeleza kwamba uchaguzi huo ulikumbwa na ghasia, rushwa na idadi ndogo ya wapiga kura waliojitokeza kupiga kura. Tume ya kupamabana na Uhalifu wa Kiuchumi na Kifedha imesema watu wasiopungua 65 walikamatwa Jumamosi kwa madai ya kuwashawishi wapiga kura.

Soma:Peter Obi kupinga mahakamani matokeo ya uchaguzi wa rais Nigeria

Kituo cha Demokrasia na Maendeleo (CDD) miongoni mwa waangalizi wa kura ya Jumamosi kimebainisha kwamba katika baadhi ya maeneo ya nchi imejitokeza hisia ya watu kuvunjika moyo ya kuona hakuna maana ya kujitokeza kupiga kura kutokana na matokeo mabaya ya uchaguzi wa rais uliomalizika. Hata hivyo CDD imesema vitengo vya kupigia kura kwingi vilifunguliwa kwa wakati na mashine za usajili wa kibayometriki zilionekana kwa kiasi kikubwa kufanya kazi ipasavyo.

Wakati huo huo, kundi lingine la waangalizi, Yiaga Africa, limepongeza maboresho makubwa katika usimamizi wa vifaa vya uchaguzi huo wa siku ya Jumamosi.

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari.Picha: Ubale Musa/DW

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari anajiandaa kuondoka madarakani mwezi Mei baada ya kuingoza nchi yake kwa mihula miwili.

Chanzo: AFP

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW