Nigeria,Syria na Cuba na hatua za Marekani
6 Januari 2010Kumezuka maoni tofauti ulimwenguni juu ya hatua ilizotangaza hivi punde Marekani ili kuimarisha usalama kwa wasafiri wa ndege wanaokwenda Marekani kutoka au kupitia nchi 14 pamoja nazo Nigeria,Somalia,Yemen, Syria, Iran,Sudan,Pakistan,Afghanistabn na Cuba.
Nigeria, imeitaka Marekani, kuuzingatia tena uamuzi wake wa kudai wasafiri wa kinigeria wachunguzwe barabara kufuatia njama ya kutaka kuiripua ndege ya Marekani siku kuu ya x-masi,mwaka jana huko Detroit,Marekani.
Katika mkutano wake na balozi wa Marekani nchini Nigeria, waziri wa nje wa Nigeria, Ojo Maduekwe,alizieleza hatua kali ilizopitisha Marekani ni "zawadi ya mwaka mpya isiokubalika".Kwani, kuanzia Jumatatu abiria wanaoruka kwa ndege kutoka Nigeria kwenda Marekani,wanapaswa kukaguliwa vile vile kama wasafiri kutoka Iran,Afghanistan au Cuba.
Hatua hizi kali zinafuatia jaribio la siku kuu ya x-masi mwaka jana ya kujiripua mnigeria Umar Farouk Abdulmutallab ambae maafisa wa usalama wa Marekani , wanaamini alipewa mafunzo ya kigaidi na tawi la Al Qaeda nchini Yemen.Katika mkutano wake na balozi wa Marekani, Bibi Robin Sanders, waziri huyo alimtaka nchi yake izingatie upya kuijumuisha Nigeria ndani ya orodha ya nchi zilizotajwa.
Orodha ya marekani inajumuisha abiria kutoka zile nchi ilizoziorodhesha kuwa etu zinaungamkono ugaidi-nazo ni Cuba,Iran,Sudan,Syria.Isitoshe, orodha hiyo inajumuisha nchi shirika kama vile Afghanistan,Algeria,Iraq,Lebanon,Pakistan,Saudi Arabia lakini pia Somalia na Yemen. Nigeria, inadai kitendo cha raia wake Abdulmutallab ,mwenye umri wa miaka 23,kisiwe mfano wa kuwahukumu wanigeria milioni 140.
Cuba,jirani na Marekani pia imekasirishwa mno kwa kuorodheshwa katika kundi hilo:Cuba ilimuita mjumbe wa kibalozi wa Marekani kisiwani Cuba kumlalamikia kuwa abiria wake wanaosafiri Marekani, wapaswa kufanyiwa ukaguzi zaidi.Cuba imezieleza hatua hizo za Marekani dhidi yake zina azma ya kisiasa ili kuhalalisha marufuku ya biashara ya Marekani inayoizingira Cuba kwa miaka 47 sasa.
Syria, nayo imjibisha hatua za Marekani za kuijumuisha katika orodha ya nchi hizo 14 kuwa hazilengi katika kuondoa hasa mzizi wa fitina: Waziri wa habari wa syria,Mohsen Bilal,aliliambia shirika la habari la Argentina,TELAM kuwa hatua za Marekani, ni sawa na " kumpa kidonge cha dawa ya asprin mgonjwa alie-mahtuti." Akaongeza waziri wa Syria kusema kwamba, huwezi kulitatua tatizo hili kwa vita,zana za kumuirika mili ya abiaria au kutunga orodha za watuhumiwa."
Hatua hizi ilisema Syria, si dawa mujarab ya kutibu maradhi ya uhalifu ulimwenguni, bali zinaleta kitisho kwetu sote bila ya kujali dini,kabila au uraia wa mtu na zinalaaniwa kote na Syria,Argentina na dunia nzima.
Abiria wa ndege waliowasili leo katika viwanja vya ndege vya Marekani chini ya hali hii ya ukaguzi mkali, wanaripoti kwamba, walikaguliwa pasi zao tena na tena na hwakuruhusiwa kutumia mabulangeti kujifunika ndani ya ndege au kuacha viti vyao vitupu saa 1 ya mwisho ya safari yao. Baadhi walisema lakini walihisi wako katika usalama zaidi.
Mwandishi: Ramadhan Ali / AFPE/RTRE
Uhariri: Othman Miraji