1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nini chanzo cha uhasama kati ya Kenya na Somalia?

24 Mei 2021

Kwa karibu miezi sita sasa, mahusiano ya kidplomasia kati ya Kenya na Somalia yalionekana kuzorota kabisa.Somalia ilichukuwa hatua za kujongelea, na Kenya ikaitikia vyema. Lakini chini chini tofauti kubwa zinasalia.

Kenia Nairobi Besuch Somalischer Präsident
Picha: picture-alliance/AP Images/K. Senosi

Siku chache baada ya uhusiano uliokuwa umeharibika kati ya Kenya na Somalia kuonekana kuboreka tena, malori ya Kenya yaliyokuwa yamejazwa miraa au mirungi yalionekana kuelekea katika uwanja wa ndege wa Wilson huko Nairobi kwa matumaini ya kuisafirisha bidhaa hiyo hadi Mogadishu.

Madereva wa malori hayo walishtushwa walipofahamishwa kwamba Kenya imepiga marufuku safari zote za kibiashara kuelekea Somalia kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia Mei 11 hadi Agosti.

Soma pia: Kenya na Somalia zakubaliana kurekebisha mahusiano

Somalia ni soko muhimu kwa miraa ya Kenya, biashara inayoiletea Kenya pato la zaidi ya dola laki moja na ishirini kila siku.

"Hatuoni mahusiano yoyote kati ya Kenya na Somalia", Hamdi Aden, mkazi wa Mogadishu aliiambia DW. "Nchi hizi mbili zinaweza kuboresha mahusiano yao ila iwapo Kenya itaendelea kuingilia wazi masuala ya Somalia, hakuna kitu kitakachoafikiwa katika muda mfupi ujao kwa ajili ya kusawazisha mahusiano."

Wanajeshi wa Kenya wakiwa tayari kwa mapambano kwenye kambi yao Tabda, ndani ya Somalia, walikopelekwa kupambana dhidi ya kundi la wanamgambo wa Al-Shabaab.Picha: Ben Curtis/AP Photo/picture alliance

Historia ya uhusiano wa mikwaruzano

Tangu uhuru, majirani hao wa Afrika Mashariki ambao baina yao wana mpaka wa kilomita 682 wamekuwa na mahusiano yasiyotabirika. Wamekuwa katika mizozo ya kimipaka, machafuko madogo maodogo na wakati mwengine nchi hizo zimehusika katika vurugu zilizosababisha umwagikaji wa damu.

Mahusiano kati ya nchi hizo yalidorora kwa kiwango cha chini zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia mnamo mwezi Novemba, pale Somalia ilipoyakata kabisa mahusiano yake ya kidiplomasia na Kenya huku ikiituhumu serikali ya Kenya kwa kuingilai masuala yake ya ndani.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alikuwa ameualika kiongozi wa kisiasa wa Somaliland, jimbo la Somalia lililojitenga na ambalo serikali kuu ya Somalia imekataa kulitambua.

Soma pia: Mzozo wa uuzaji miraa kati ya Kenya na Somalia

Hatua hiyo ilipelekea kufukuzwa kwa balozi wa Kenya nchini Somalia na balozi wa Somalia nchini Kenya akaagizwa kurudi nyumbani na Rais Abdullahi Farmajo.

Kenya imekanusha kuyaingilia masuala ya ndani ya Somalia na kudai kwamba Rais Farmajo anatumia suala hilo kama kisingizio ili apate uungwaji mkono wa kisiasa nchini mwake.

Ramani ikionesha mipaka ya bahari kati ya Kenya na Somalia pamoja na maeneo yanayozozaniwa.

Mwasisi na mshauri wa kimkakati wa shirika la Sahan ambalo linajihusisha na masuala ya amani na usalama katika Pembe ya Afrika Matt Byden, anasema, suala kuu hasa ni mzozo wa ndani ya Somalia kuhusiana na eneo linalotawaliwa na madola mawili.

Kambi ya Daadab na mzozo wa bahari kama nguvu ya wenzo?

Kenya imekuwa mwenyeji wa maelfu ya wakimbizi kutoka Somalia tangu kuondolewa madarakani kwa dikteta Siad Barre mwaka 1991.

Lakini Rais Uhuru Kenyatta mara kadhaa ametishia kuifunga kambi ya wakimbizi ya Dadaab ambayo inadaiwa kuwa kambi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani.

Utawala wa Kenyatta umeupatia Umoja wa Mataifa hadi Juni mwakani kuwatafutia makao mapya wakimbizi wa Somalia nchini humo.

Kenya na Somalia pia ziko katika mzozo wa muda mrefu wa mpakani katika Bahari ya Hindi, eneo linaloaminika kuwa na hifadhi kubwa ya mafuta na gesi. Mzozo huo kwa sasa uko katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ.

Mwandishi wa DW mjini Mogadishu Mohammed Odowa anasema nchi hizi mbili zinastahili kupunguza mivutano na kuingia katika mazungumzo ili matatizo haya yaliyoko yapatiwe ufumbuzi.

Chanzo: DW

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW