1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nini kinachochea ushawishi wa Urusi barani Afrika?

11 Februari 2022

Ushawishi wa Urusi barani Afrika umeongezeka katika miaka ya karibuni. Urusi imejipenyeza hasa katika mizozo ya barani humo kuanzia mamluki wanaosaidia na waasi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, na pia nchini Mali.

Russland | Treffen Emannuel Macron und Wladimir Putin
Picha: Russian Presidential Press Office/SNA/imago images

Wachambuzi wengi wanashawishika kuwa maslahi mapya ya Urusi barani Afrika yanatokana na jukumu linaloongezeka la Afrika katika masuala ya ulimwengu, ukuaji wa kasi wa uchumi na maendeleo ya teknolojia yanayoshuhudiwa katika baadhi ya nchi za bara hilo. Afrika inaonekana pia kuwa eneo jipya la ukuaji uchumi, uwekezaji na biashara. Zaidi ya hayo, Moscow taratibu inageukia Afrika ili kudhihirisha nguvu na ushawishi.

Urusi imekuwa mshirika wa nchi kadhaa za Kiafrika katika mapambano yao na waasi. Nchi tano za ukanda wa chini wa jangwa la sahara – Mali, Niger, Chad, Burkina Faso na Mauritania – ziliiomba Moscow mwaka wa 2018 kuyasaidia majeshi yao na vikosi vya usalama kupambana na kundi linalojiita Dola la Kiislamu – IS na al-Qaeda.

Lakini matumizi ya mamluki wa Urusi yanasababisha mipasuko ya ndani na kuwatenga washirika wengine wa nje. Kwa mujibu wa Taasisi ya imataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm - SIPRI, Afrika iliachangia asilimia 18 ya mauzo yote ya silaha za Urusi kati ya 2016 na 2020, na Algeria ndiyo iliyonufaika Zaidi na biashara hiyo.

Putin na rais wa Namibia Hage GeingobPicha: Mihail Mokrushin/dpa/picture alliance

Lakini ni nini mpango wa Urusi kisiasa na kiuchumi? Vipi madola ya Ulaya yanashughulikia hilo? Na nini Urusi inataraji kunufaika kutokana na kuhusika kwake pakubwa barani humo?

Zaidi ya dazeni ya washirika wa Magharibi wamelaani kile wanachosema ni kupelekwa mamluki wa Urusi nchini Mali. Wanasema hatua hiyo inaweza "ikaharibu hata Zaidi hali ya usalama katika eneo la Afrika Magharibi”, ambalo linapambana na makundi ya itikadi kali.

Mataifa 15 ya Ulaya na Canada yaliituhumu Urusi kwa kutoa msaada wa vifaa kwa kupeleka mamluki kutoka kampuni ya Wagner. Urusi inakanusha kuwa na mahusiano yoyote ya kiserikali na kampuni hiyo ya kinbinafsi ya kijeshi.

Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Christine Lambrecht anasema jeshi la Ujerumani – Bundeswehr halitojiondoa katika taifa la Afrika Maghaeribi na Mali lililoharibiwa kwa vita, kama kampuni ya mamluki ya Urusi itaendelea kuhudumu nchini humo.

Faustin Archange Touadera na Putin Picha: Sergei Chirikov/AP Photo/picture alliance

Mkutano wa kilele wa 2019 kati ya Urusi na Afrika, wa kwanza wa aina yake, uliandaliwa Sochi na kuhudhuriwa na wakuu wa mataifa 43 ya Afrika. Inafahamika wazi kuwa Muungano wa Kisovieti ulizipa msaada nchi kadhaa za Kiafrika wakati wa mapambano ya kupinga ukoloni.

Putin alizuru bara hilo mwaka wa 2006, na kuahidi dola bilioni moja katika uwekezaji na kufanya tamko la wazi la maslahi ya Urusi. Kufikia mwaka uliofuata, Urusi ilikuwa imefuta karibu madeni ya dola bilioni 20 iliyozidai nchi za Afrika wakati wa Vita Baridi.

Urusi ilisaini Mkataba wa Ushirikiano Mpana wa Kimkakati na Afrika Kusini, katika maeneo ya kisiasa, kiuchumi na ulinzi.

Mahusuano ya ulinzi kati ya Urusi na Afrika pia yanakuwa. Tangu mwaka wa 2014, Rosoboronexport - shirika la serikali linalouza nje vifaa vya kijeshi na huduma – limesaini makubaliano ya pande mbili na nchi kadhaa za Afrika, zikiwemo Angola, Guinea ya Ikweta, Mali, Nigeria na Sudan. Kando na vifaa vya kijeshi, makubaliano hayo yanahusisha pia kupambana na ugaidi mafunzo ya Pamoja ya wanajeshi.

Urusi pia ina malengo ya kiuchumi wakati linapokuja suala la maliasili. Ijapokuwa ina utajiri wake wa madini, ni kazi ngumu kuyachimba madini na kwa hiyo inakuwa rahisi kununua kutoka nje. Kuna uchimbani wa madini ya platinum Zimbabwe, almasi nchini Angola na urani nchini Namibia.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW