1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nini kitarajiwe baada ya Israel kulivunja bunge?

30 Mei 2019

Israel imejikuta katika hali ya kisiasa ambayo haijapata kushuhudiwa baada ya kuvunjwa kwa bunge jipya na hivyo kulazimika kupanga tarehe mpya ya uchaguzi katika kipindi cha miezi sita. Nini kinafuata baada ya hapo? 

Symbolbild Neuwahlen in Israel
Picha: AFP/Getty Images/J. Guez

Ni siku 50 tu baada ya kuonekana kupata ushindi wa kuridhisha, na kupata nafasi ya kuchaguliwa tena, waziri mkuu Benjamin Netanyahu amekiri kushindwa kuunda serikali ya kitaifa na kulazimika kuitisha uchaguzi mwingine kupitia bunge. Baada ya mshirika wake wa zamani Avigdor Lieberman kulivunja kundi la siasa kali za kizalendo lililomuunga mkono Netanyahu kwa muda mrefu, bado haiko wazi iwapo uchaguzi huo wa pili utatoa matokeo yatakayomaliza mkwamo.

Kwa namna yoyote, hatua hiyo inaiweka Israel katika wakati mwingine mgumu wa kampeni za miezi mitatu na nusu, muda mfupi tu baada ya kuhitimisha zile za awali.

Rais wa Israel Reuven Rivlin anakabiliwa na kibarua cha kufanikisha mchakato wa kuundwa kwa serikali mpya.Picha: Getty Images/AFP/M. Kahana

Kipi kinatarajiwa?

Tangu Netanyahu aliposhindwa kuunda serikali ya kitaifa katika muda anaopewa kisheria, na kutotaka kumpa fursa hiyo mpinzani wake mkuu, aliyewahi kuwa mkuu wa majeshi Beny Gantz, alishinikiza muswada wa sheria kulivunja bunge ili kuitisha upya kampeni za uchaguzi.

Tarehe mpya ya uchaguzi iliyopangwa ni Septemba 17. Vyama vya siasa vinavyoshiriki hivi sasa vinalazimika kuchagua viongozi pamoja na wagombea wa ubunge na kuanza kampeni ambazo huwa ni za gharama kubwa.

Baada ya uchaguzi huo mpya wa Septemba, mchakato uleule utaanza tena. Rais wa Israel atatakiwa kuchagua mgombea wa uwaziri mkuu, mwenye nafasi nzuri ya kuunda serikali imara ya muungano. Mgombea atakuwa na siku 42 za kuunda serikali, na iwapo atashindwa, rais ana uwezo wa kutafuta mgombea mwingine na kumpa siku 28 kuunda muungano mbadala ama kutangaza kushindikana kuundwa kwa serikali ya muungano na kuitisha uchaguzi mpya kabla ya kuundwa kwa serikali- kitu ambacho hakijawahi kutokea katika historia ya Israel.

Na sheria je, imemkalia vipi Netanyahu?

Mwanasheria mkuu wa serikali anataka Netanyahu kufunguliwa mashitaka na kumuweka kwenye hali ngumu ya kusalia mamlakani.Picha: Getty Images/AFP/J. Guez

Mwanasheria mkuu wa serikali nchini Israel amependekeza kufunguliwa kwa mashitaka ya jinai dhidi ya Netanyahu, akitaka afunguliwe mashitaka matatu tofauti ya ufisadi, kukisubiriwa vikao vya kabla ya kuanza kwa kesi yenyewe. Mashitaka hayo ni pamoja na kukubali zawadi kutoka kwa marafiki zake mabilionea pamoja na kutengeneza kanuni zitakazoinufaisha kampuni kubwa ya mawasiliano, ili asiandikwe vibaya na vyombo vya habari. Mashitaka haya, hatimaye yataanza kusikilizwa mapema mwezi Oktoba. 

Hata kama atashinda kwenye uchaguzi wa Septemba, kuna uwezekano mdogo kwa Netanyahu kupata uungwaji mkono wa kisiasa unaotakiwa, ili kupata kinga anayoitarajia kabla ya kesi inayomkabili. Kwa hivyo, hatakuwa na namna ya kukwepa kusimama kizimbani, hali itakayoongeza shinikizo dhidi yake la kuachia madaraka.

Na kuhusu mpango wa amani,

Rais Donald Trump  wa Marekani, anayefurahia mahusiano ya karibu kabisa na Netanyahu, aliapa kuzindua mpango wake wa amani katika eneo la Mashariki ya Kati baada ya uchaguzi wa Israel. Marekani, imepanga mkutano mwezi ujao huko Bahrain utakaozindua awamu ya kwanza ya mkakati wa uwekezaji katika maeneo ya Palestina. Lakini bado haiko wazi ni kwa namna gani mzozo wa kisiasa wa karibuni utakavyoathiri kuzinduliwa kwa mpango huo.   

Washauri wa rais Trump kuhusu masuala ya Mashariki ya Kati, Jared Kushner na Jason Greenblatt watakwenda Israel siku ya Alhamisi baada ya ziara ya Trump nchini Jordan, ambako atakuwa akitafuta uungaji mkono wa mataifa ya kiarabu katika mkutano huo wa amani.

Jordan imesema kwa mara nyingine kuwa inaamini katika suluhu ya mataifa mawili, na kuundwa kwa taifa huru la Palestina pamoja na Israel, jambo linaloonekana kutofautiana na kile kinachotajwa kama "Mpango wa karne wa Trump unaosubiri kuzinduliwa.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW