1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Njaa inayohusiana na Covid-19 huua watoto 10,000 kwa mwezi

29 Julai 2020

Umoja wa Mataifa unasema virusi vya corona na hatua za kuzuwia kusambaa kwake vinaziadhibu jamii zinazokabiliwa tayari na njaa, na kusababisha vifo vya takribani watoto wadogo zaidi ya 10,000 kwa mwezi.

Venezuela Mangelernährung Kinder
Picha: Reuters/C. G. Rawlins

Katika maeneo maskini ya dunia, janga la virusi vya corona linafunika tatizo lingine: ambalo ni njaa. Vizuwizi vya kusafiri na hofu ya covid-19 vimefanya iwe vigumu kwa wagonjwa kwenda hospitali, na pia kuvuna mazao.

Dk. Coumbo Boly, daktari wa watoto katika hospitali ya chuo kikuu cha Yalgado Ouedrago, nchini Burkina Faso, anahofia wimbi linalokuja na njaa.

"Tulikuwa tunataraji idadi ya watoto wenye utapiamlo kuongezeka kwa mara mbili, tatu au hata tano kwenye mwezi wa Novemba na Desemba, wakati ambapo kawaida ni msimu wa mavuno. Lakini, asiepanda hawezi kuvuna," anasema.

Katika baadhi ya maeneo, utapiamlo tayari unaongezeka. Masaa manne kuelekea kusini mwa Burkina Faso, katika mkoa wa Tuy, mtoto Haboue Solange mwense umri wa mwezi mmoja, tayari amepoteza nusu ya uzito wake wa mwili. Mama yake pia anakabiliwa na utapiamlo mkubwa kiasi cha kushindwa hata kuzalisha maziwa ya kumnyonyesha.

Soma zaidi 450,000 waambukizwa korona, 7,000 wafa Afrika Kusini

Vizazi vya watoto walio chini ya uzito vinaripotiwa kuwa juu kwa asilimia 40 mkoani Tuy, moja ya maeneo yanayoongozwa kwa mavuno ya nafaka nchini humo. Katika matifa yanayokabiliwa na vita na ukame, mporomoko wa kiuchumi uliosababishwa na janga la virusi vya corona umeongeza madhila juu ya madhila.

Mtoto mwenye ugonjwa wa utapiamlo akipimwa uzito kwenye wadi ya wagonjwa wa utapiamlo kwenye hospitali ya al-Sabeen mjini Sanaa.Picha: Reuters/K. Abdullah

Idadi ya waliodhoofika yapanda zaidi

Umoja wa Mataifa unasema watoto wasiopata lishe bora wanakufa kwa kiwango cha karibu 10,000 kwa mwezi kote duniani. Idadi ya watoto waliokumbwa na ugonjwa wa kudhoofika imeongezeka kwa karibu milioni 7 kutoka mwaka uliopita.

David beasley, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa - WFP, hivi karibuni aliliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba dunia iko kwenye kingo za janga la njaa.

Unaweza kusoma pia Kenyatta aongeza tena vizuizi dhidi ya corona

"Niko hapa kwa ajili ya kutoa onyo. Bado hakujawa na ukame. Lakini laazima niwaonye kwamba ikiwa hatutajiandaa na kuchukuwa hatua sasa kuhakikisha upatikanaji wa chakula, kuepusha nakisi ya ufadhili na uvurugaji wa biashara, tunaweza kukabiliwa na ukame wa kiwango kikubwa sana katika muda wa miezi michache."

Hakuna njia kwa wagonjwa kufika hospitali

Nchini Afghanistan, vizuwizi vya usafiri na hofu ya virusi vya corona vinamaanisha kuwa watoto wachache sasa wanasafiri kutoka mikoa kwenda katika hospitali za watoto, kama hospitali ya watoto ya Indira Ghandi iliyoko mjini Kabul.

Dr. Nematullah Amir, anasema watoto wenye utapiamlo wanaolazwa hospitalini hapo wamepungua kutoka kati ya 30 na 40 mwaka uliyopita hadi 14.

Hata kabla ya covid-19,  kulikuwa na takribani watoto milioni 47 wenye umri wa chini ya miaka mitano waliodhoofika kwa kiwango cha wastani au kibaya, wengi wao kutoka eneo la Afrika kusini mwa Sahara na kusini-mashariki mwa Asia.

Na sasa, wakti ambapo hatua za vizuwizi na njia za kimataifa za biashara zikiruga ugavi muhimu wa misaada, Umoja wa Mataifa unaonya kuwa janga la virusi vya corona, huenda likasababisha athari ya kizazi kwa afya ya mamilioni.

Chanzo: Mashirika

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW