1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Njaa na mgogoro wa fedha duniani

L.Schadomsky - (P.Martin)15 Oktoba 2008

Kwa mujibu wa Umoja wa Ulaya,serikali za umoja huo zimejitolea kulipa takriban Euro trilioni mbili katika jitahada ya kutuliza masoko yake ya fedha.Ujerumani peke yake,itatoa kama bilioni 500 kusaidia benki zake.

Shirika la Kijerumani linalotoa misaada ya chakula duniani, likizingatia mabilioni yanayotolewa kwa benki mbali mbali kuimarisha masoko ya hisa, limetoa wito wa kuwepo mpango maalum utakaosaidia kutekeleza Malengo ya Milenia kupunguza kwa nusu idadi ya watu wenye njaa,ifikapo mwaka 2015.

Katika majuma yaliyopita,mara kwa mara wanasiasa wa nchi zinazoendelea walikuwa wakiuliza,yawezekanaje kwa nchi tajiri zilizoendelea kiviwanda kutoa mabilioni katika muda wa siku chache tu,lakini husahau kutimiza ahadi za kusaidia nchi zinazoendelea? Hilo ni suala lililozuka pia kwenye mikutano ya hivi karibuni ya Shirika la Fedha Duniani IMF na Benki ya Dunia.Kwani kuna hofu kuwa kundi la nchi tajiri ambazo bado hazijatimiza ahadi zilizotolewa,huenda likapunguza zaidi matumizi yake.

Kwa upande mwingine,kuna sababu za kuwa na matumaini hata kama idadi ya nchi masikini imefikia 33.Kwani bei za mazao ambazo kwa wastani ziliongezeka kwa asilimia 60 na hata asilimia 300 kwa zao la ngano huko Somalia,sasa zimepunguka kwa kiwango kikubwa.Lakini hazitorejea kwenye bei za hapo awali.Vile vile miradi mingi ya miundombinu katika nchi zinazoendelea kwa sehemu kubwa inagharimiwa na Benki ya Dunia na sio nchi fadhili moja moja.Na hivi karibuni Benki ya Dunia ilisisitiza kuwa haina shida kuongeza maradufu viwango vya mikopo yake.Hatimae,msaada wa maendeleo siku hizi ni fahari ya kitaifa.Kwa hivyo haitofaa kwa nchi kama Ujerumani kulega nyuma katika utekelezaji wa ahadi zake.

Mambo hayo yote hudhihirisha kuwa mgogoro wa fedha hautoathiri moja kwa moja nchi zinazoendelea.Kitakachoathiri uchumi wa nchi hizo ni kupunguka kwa fedha zinazopelekwa nyumbani na wananachi wake wanaoishi nje pamoja na kupunguka kwa uwekezaji na idadi ya watalii kutoka nchi tajiri.

Kwa upande mwingine nchi zinazoendelea zinapaswa kuwajibika pia.Kwa mfano zingetoa asilimia 10 ya bajeti ya taifa kuendeleza sekta ya kilimo. Hivi sasa kiwango hicho ni asilimia 4 tu.Vile vile wakulima wasiwekewe vipingamizi wanapojaribu kujipatia ardhi au mikopo midogo dogo,hali inayokutikana huko Ethiopia ikiwa ni nchi mojawapo inayokumbwa na njaa.