Njama ya kutaka kumuuwa rais Sheikh Sharif Ahmed wa Somalia
22 Oktoba 2009Watu wasiopungua 30 wameuwawa na zaidi ya 58 kujeruhiwa mjini Mogadischu katika mapigano kati ya vikosi vya Umoja wa Afrika na waasi wa kisomali waliofyetua makombora dhidi ya ndege ya rais.
Ni mapigano makali kabisa kuwahi kushuhudiwa tangu wiki kadhaa zilizopita, katika mji mkuu wa Somalia Mogadischu.
Mashahidi wanasema kwamba waasi walifyetua makombora kuelekea uwanja wa ndege wa kimataifa katika wakati ambapo rais Sheikh Sharif Ahmed alikua anaelekea Uganda kuhudhuria mkutano wa viongozi wa umoja wa Afrika kuhusu wakimbizi .Rais Sharif Ahmed hajadhurika.
Wanajeshi wa Somalia wakisaidiwa na wanajeshi wa Umoja wa Afrika wamejibisha hujuma hizo kwa kuripua mizinga.
Makombora ya waasi yameangukia katika maeneo wanakoishi raia wa kawaida na hata sokoni.
Farah Olow,mfanyabiashara katika markiti ya Bakara ameliambia shirika la habari la Reuters watu sita wamepoteza maisha yao, kombora lilipopiga katika nyumba yao.
"Watu wanakimbilia ndani ili kuyanusuru maisha yao-lakini haisaidii kitu.Hatuwezi kusema idadi halisi ya waliokufa,mvua ya mizinga bado inanyesha." amesema mfanyabiashara huyo.
Ushahidi kama huo umetolewa na mfanyabiashara mwenzake Ahmed Abdullahi Gobe aliyeliambia shirika la habari la AFP,"watu wengi wamekufa sokoni.Risasi zimeanza kufyetuliwa wakati watu walipokua wakianza harakati zao za kila siku za kimaisha.Soko lilikua limesheheni watu",amesema mfanyabiashara huyo na kuongeza tunanukuu:"Sijawahi kuona msiba kama huu tangu muda mrefu uliopita."Mwisho wa kumnukuu.
Serikali ya mpito ya Somalia inayoungwa mkono na Umoja wa mataifa inakabiliwa na mtihani wa waasi wa itikadi kali ya dini ya kiislam,na hasa wapiganaji wa Al Shabab.
Muungano wa waasi wa Al Shabab wanaofuata nyayo za magaidi wa Al Qaida na kundi la Hezb-al Islam walifanya mashambulio makubwa May 7 iliyopita kote nchini Somalia kwa lengo la kutaka kumpindua Sheikh Charif Ahmed anaelindwa na vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Afrika AMISOM.
Mji mkuu wa Somalia-Mogadischu ulikua tulivu kidogo tangu mapema mwezi huu,hasa baada ya makundi mawili ya waasi kuanza kupigana wenyewe kwa wenyewe kuania mji wa bandari wa Kismayu,kusini mwa Somalia.
Vichwa mchungu wa upande wa upinzani nchini Somalia wamekua kila wakati wakifanya mashambulio kwa hoja kwamba Somalia ingali bado inakaliwa na wanajeshi elfu tano wa kutoka Uganda na Burundi wanaotumikia kikosi cha kulinda amani cha umoja wa Afrika.
Mapigano nchini Somalia yameshagharimu maisha ya zaidi ya raia 19 elfu na kuwatimua zaidi ya milioni moja na nusu majumbani mwao tangu yaliporipuka upya mnamo mwaka 2007.
Mwandishi:Oummilkheir Hamidou /AFP/Reuters
Mhariri:Abdul-Rahman