Njia za maambukizi na kinga
5 Desemba 2014Mambukizi ya Ebola kutoka mtu mmoja hadi mwengine ni kupitia maji maji mwilini mfano kushika damu, mate, jasho au mbegu za uzazi kutoka kwa mtu aliyeambukizwa. Watu wengi wanaoambukizwa tangu kuzuka kwa mripuko wa sasa wa Ebola katika mataifa ya Afrika Magharibi, ni kupitia moja wapo ya njia hizi. Madaktari na watu wanogusana kimwili na waathiriwa wa Ebola wamo hatarini zaidi.
Njia nyingine za kuambukiza:
- Kupitia tendo la ngono
- Kwa kushika maiti ya muathirika
- Kwa kushika vitu au sehemu zilizoshikwa na watu walioathirika, mfano muathiriwa anaposhika mlango baada ya kujifuta machozi.
Watafiti wanasema kuwa popo ni mnyama anayeweza kusambaza virusi hivi haraka na kwa urahisi sana, yaani ni kama Ghala la Virusi vya Ebola. Sokwe pia ana uwezo wa kuhifadhi virusi hivi vya Ebola na ni rahisi kusambaza virusi mtu anapogusana na mnyama huyu aliyeambukizwa virusi au kula Nyama ya mwituni. Pia Panya ni hatari kwani anauwezo wa kubeba virusi na kuvisambaza kwa haraka sana. Yaaminika kisa cha kwanza cha Ugonjwa wa Ebola kilitokana na mwanadamu kula nyama ya mmoja wa wanyama hawa waliotajwa.
Hadi kufikia sasa hakuna ushahidi wowote kwamba ugonjwa wa Ebola unaweza kusambazwa na mbu au wadudu wengine.
Ni muhimu kufahamu kwamba mtu hawezi kuambukiza au kusambaza virusi vya ugonjwa huu wa Ebola hadi dalili za kwanza za ugonjwa huu zinapoanza kuonekana.
Usafi wa mtu binafsi ni kinga bora dhidi ya ugonjwa huu. Kunawa mikono kila mara na sabuni, maji yaliyochanganywa na klorini na kemikali za kuua viini, ni miongoni mwa hatua za kuzuia kusambaa kwa ugonjwa huu hasa katika mataifa yanayoathirika zaidi. Nchini Liberia, Sierra Leone na Guinea, matangi ya maji yaliyochanganywa na klorini yamewekwa katika kila jengo linalotoa huduma za umma huku watu wakiwa hawasalimiani tena kwa mikono au kukumbatiana hasa katika sehemu nyingi ambako ugonjwa huu umezuka, na badala yake kubuni mitindo mipya ya kusalimiana pasi na kushikana mikono.
Kuvaa glovu na mavazi rasmi ya kufunika uso, sio hakikisho la asili mia kwa mia ya kinga dhidi ya ugonjwa huu, ila mavazi haya yanaweza kusaidia kukinga iwapo yatatumiwa kwa njia ipasayo. Lakini mtu anahitaji kupata mafunzo maalum, na kuyavua baada ya kumhudumia mgonjwa aliyeambukiza au kufanya kazi katika maeneo hatari. Mavazi haya yanapasa kuvuliwa kisha kuchomwa mara moja baada ya kutumika.
Kanuni unazopasa kuzingatia katika maeneo yanayokumbwa na ugonjwa wa Ebola:
- Kuepuka kugusana kimwili na watu au vitu
- Usifute uso wako kwa mikono
- Nawa mikono mara kwa mara!
Virusi vya Ebola vinaweza kuingia mwilini kupitia vidonda, macho, mdomo au tundu nyingine za mwilini.