1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

[No title]

19 Desemba 2006

Ahmedou Ould Abdallah atafikisha ujumbe wa katibu mkuu wa umoja wa mataifa kwa rais huyo wa Sudan juu ya mapendekezo ya kutanzua mzozo huo wa Darfur.

Koffi Annan ambaye anaondoka ofisini mwishoni mwa mwaka huu kumpa nafasi mrithi wake Ban-ki Moon, amemteua mujumbe huyo maalum ambaye ni afisa wa juu katika umoja wa mataifa.

Mbali naye pia Koffi Anan amemteua waziri wa zamani wa mambo ya nchi za nje wa Sweeden Jan Eliason, katika timu maalum ya umoja wa mataifa ikiwa na nia ya kuishawishi serikali ya Sudan ikubali majeshi ya kimataifa kulinda aman huko Darfur.

Elliason ambaye mapema mwaka huu alijiuzulu wadhifa wa rais wa baraza la usalama la umoja wa mataifa , amesema jukumu lake ni kusaidia juhudi za kidiplomasia kufikia makubaliano na serikali ya Sudan, kuruhusu jeshi la kimataifa kwenda Darfur.

Mjini Washinton, mjumbe wa marekani katika mzozo huo wa Sudan, Andrew Natsios amesema kuwa tarehe mosi January ni tarehe ya mwisho kwa serikali ya Sudan kukubaliana na jeshi la umoja wa mataifa pamoja na lile la umoja wa afrika kuingia Darfur.

Natsios amesema kuwa Serikali ya Sudan inabidi iamua moja kukubaliana na pendekezo hilo, au vinginevyo kuwa tayari kukabiliana na njia nyingine ambayo hakuitaja zaidi ya kusema mpango mwengine.

Hayo yakiendelea, umoja wa ulaya hii leo umetangaza msaada zaidi kwa wahanga wa mauaji ya hujko Darfur, huku wakiitaka serikali ya Sudan na viongozi wa waasi kurejea katika meza ya mazungumzo.

Kamishna wa umoja huo Louis Michel amesema kuwa msaada huo uliyoongezwa ni wa kiasi cha dola millioni 22.

Amesema hali ilivyo hivi sasa huko Darfur ni mbaya kwa maisha ya binaadam, na kwamba umoja wa ulaya utaendelea kusaidia kupatikana kwa muafaka kwa njia ya amani.

Lous amelaani wazo la kuutanzua mzozo huo kwa njia ya kijeshi kuwa ni mawazo ya kijinga na kwamba ni ishara ya kutoona mbali.

Serikali ya Sudan ambayo imekataa kupelekewa kwa walinda amani wa umoja wa mataifa, pia inapinga wazo la kupelekwa kwa jeshi la muungano wa umoja wa afrika na umoja wa mataifa.

Hivi sasa kuna kiasi cha askari 7,000 wa umoja wa afrika huko Darfur ambao wanakabiliwa na uhaba wa fedha na nyenzo duni.

Zaidi ya watu laki mbili wameuawa na wengine kiasi cha millioni 2 hawana makazi kutokana na vita hivyo vya takriban miaka minne huko Darfur ambavyo sasa vimesambaa hadi nchi jirani ya Chard.