Norway kuwapokea wahamiaji 600 waliopelekwa Rwanda
9 Januari 2020Norway mwaka huu itawachukua watu 600 waliopelekwa nchini Rwanda kutoka katika vituo vya kuwashikilia nchini Libya , nchi hiyo imesema Jumatano wakati ikitafuta kukatisha tamaa juhudi za kuwasafirisha watu kwa njia haramu kupitia bahari ya Mediterania.
Rwanda, ambako zaidi ya watu milioni 2 walikimbia makaazi yao kutokana na mauaji ya kimbari mwaka 1994, ilitia saini makubaliano na Umoja wa Mataifa mwezi Septemba yenye lengo la kusaidia kuwapa makaazi watu walioshikiliwa nchini Libya wakati wakijaribu kusafiri kwenda Ulaya.
Wahamiaji waliopelekwa nchini Rwanda wamepewa hadhi ya waomba hifadhi katika nchi hiyo wakati shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCR likiamua iwapo ni wakimbizi. Katika taarifa kwa shirika la habari la Reuters, waziri wa sheria wa Norway Joeran Kallmyr amesema idadi ya watu watakaochukuliwa mwaka 2020 ni 600, lakini aliongeza kuwa hiyo haitaelekeza katika ongezeko ya idadi jumla ya wakimbizi ambao serikali iliyopita ilidhamiria.