NOUAKCHOTT. Mawaziri wa Umoja wa Afrika wazungumza na wanamapinduzi
10 Agosti 2005Mawaziri wa umoja wa nchi za Afrika wamefanya mazungumzo na utawala mpya wa kijeshi nchini Mauritania.
Wanajeshi wa Mauritania walimpindua rais Maaya Sid Ahmed Ould Taya katika mapinduzi yasiyokuwa na umwagikaji damu.
Umoja wa Afrika umelaani mapinduzi hayo na ukachukua hatua ya kuiondolea Mauritania uanachama wake wa umoja wa Afrika.
Umoja wa Afrika unataka Mauritania irejeshwe katika hali ya utengamano lakini haupigi tena debe la kutaka rais aliyepinduliwa arejeshwe mamlakani.
Rais huyo aliyeitawala Mauritania kutoka mwaka 1984 hakuwa tena na umaarufu nchini mwake na raia wengi wameunga mkono mapinduzi hayo.
Utawala wa kijeshi umeahidi kuachia madaraka baada ya miaka miwili wakati ambapo nchi hiyo itakuwa imekamilisha katiba mpya, uchaguzi wa bunge pamoja na wa urais.