Ntanganda yuko korokoroni ICC
23 Machi 2013Ntaganda amejisalimisha mwenyewe ili kuruhusu akabiliane na madai ambayo ni pamoja na mauaji, ubakaji na kuwatumia watoto kama wanajeshi.
Mtuhumiwa wa kwanza kuweza kujisalimisha binafsi kwa mahakama hiyo ya ICC, Ntaganda anatakiwa kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu, madai ambayo anadaiwa yalifanyika wakati akiwa mbabe wa kivita katika eneo la mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
Ajisalimisha katika ubalozi wa Marekani
Aliingia katika ubalozi wa Marekani nchini Rwanda siku ya Jumatatu na aliomba apelekwe katika mahakama hiyo mjini The Hague.
Ntaganda anadai kuwa alihusika katika mauaji ya kinyama ya kiasi ya watu 800 katika vijiji katika eneo lenye matatizo la mashariki ya Kongo. Pia anatuhumiwa kuwatumia watoto kama wanajeshi katika jeshi lake la waasi na kuwaweka wanawake kama watumwa wa ngono kati ya Septemba mwaka 2002 na Septemba mwaka 2003.
Alipelekwa katika mahabusu ya ICC mjini Kigali na kusafirishwa hadi katika uwanja wa ndege wa mjini Rotterdam. Mahakama ya ICC ilisema katika ukurasa wake wa Tweeter baada ya Bosco Ntaganda aliwasili katika kituo cha kuwahifadhi watuhumiwa cha ICC, akiwa chini ya ulinzi wa polisi wa Uholanzi katika kitongoji cha mji wa The Hague cha Scheveningen.
Ntaganda, ambaye amezaliwa mwaka 1973, atakuwa Mwafrika wa tano kuingia katika mahabusu ya ICC. Atakabiliana na majaji kwa mara ya kwanza siku ya Jumanne, baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kiafya.
Majaji watathibitisha utambulisho wake na lugha ambayo ataweza kufanya mawasiliano ili kuweza kuelewa yale yanayozungumzwa mahakamani na pia atafahamishwa mashtaka dhidi yake, mahakama hiyo imesema.
Bensuda afurahishwa
Mwendesha mashtaka mkuu wa ICC, Fatou Bensouda amekaribisha taarifa hizo za kusafirishwa kwa Ntanganda, akisema kuwa "Hii ni siku nzuri sana kwa wahanga katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na pia kwa sheria za kimataifa. Leo wale ambao wanadaiwa kuwa waliteseka kutokana na Bosco Ntaganda wanaweza kuwa na matumaini juu ya uwezekano wa sheria kuchukua mkondo wake," amesema katika taarifa.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, John Kerry amesifu kuwa hiyo ni hatua kubwa iliyopigwa, "kwa sheria na uwajibikaji." "Sasa yapo matumaini kuwa haki itatendeka," amesema katika taarifa.
Kuwasili kwa Ntaganda mjini The Hague "pia kutatoa ishara nzito kwa wale wote wanaotenda vitendo vya kinyama kuwa watawajibishwa kwa uhalifu wao," Kerry amesema.
Geraldine Mattioli-Zeltner wa shirika la Human Rights Watch , amesema kuwa kuwasili kwa Ntaganda katika mahakama ya ICC " kutakuwa ushindi mkubwa kwa wahanga wa mauaji mashariki mwa Kongo na wanaharakati wa eneo hilo ambao wamefanya kazi katika hali ya tahadhari kubwa kwa ajili ya kukamatwa kwake.
Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Grace Patricia Kabogo