NTC yakabidhi madaraka Libya
9 Agosti 2012"Ninakabidhi madaraka ya kikatiba kwa Bunge la nchi hii, ambalo kuanzia sasa ndicho chombo kinachowawakilisha watu wa Libya". Ni kauli ya Kiongozi wa Baraza la Mpito nchini Libya Mustafa Abdel Jalil.
Jalil ametoa kijiti cha uongozi kwa wabunge wapatao 200 kutoka kwenye vyama vya siasa na wabunge wa kujitegemea waliochaguliwa tarehe 7 mwezi uliopita. Kwa heshima ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, sherehe za kukabidhi madaraka zilifanyika usiku hapo jana baada ya futari. Muda mfupi kabla ya tukio hilo wabunge hao waliapishwa na Rais wa mahakama kuu nchini humo.
Kiongozi huyo ameiita hatua hiyo kuwa ni ya kwanza kuwahi kushuhudiwa katika historia ya taifa hilo na kwamba ni tukio la kihistoria kwa Walibya wote. Pamoja na kutimiza wajibu huo wa kidemokrasia, Jalil amekiri kuwa kipindi cha mpito kimefanya makosa kwani masuala ya ulinzi na upunguzaji wa silaha hayakupatiwa suluhu katika muda muafaka.
Makosa ya NTC
Amesema kuwa NTC pia limefeli kutafuta suluhu ya tatizo la wakimbizi ambao kwa mtazamo wake ni janga kubwa linaloikabili nchi hiyo. Jalil anafafanua na hapa ninamnukuu "hatukuweza kuwahakikishia ulinzi wananchi wa Libya kama tulivyotaka na pia kama walivyotaka wao" mwisho wa kumnukuuu.
Kiongozi huyo alitangaza pia kuachia nafasi yake ya kuongoza NTC pamoja na jopo la mahakimu ambalo amekuwa mwanachama tangu enzi za utawala wa Gaddafi.
Jana ambapo Ramadhani 20 ni ya kihistoria kwa Walibya si tu kwa NTC kukabidhi utawalawa kwa bunge. Mwaka uliopita siku kama hiyo ya mfungo 20 waasi waliuchukua mji mkuu wa Tripoli kitendo kilichomlazimisha Gaddafi kukimbia.
Chumba cha mkutano kwenye hoteli pembezoni mwa mji mkuu wa Tripoli ndicho kitakachotumika na bunge hilo katika shughuli zake ambazo zinatarajiwa kuanza wiki moja kutoka sasa. Chumba kingine kitatumika kama makao makuu ya bunge hilo. Hii leo bunge hilo litamchagua Rais wake kupitia kura.
Majukumu ya bunge
Mojawapo ya majukumu ya bunge hilo ni kumchagua Waziri Mkuu ambaye ataunda serikali hatua ambayo itafanyika mara baada ya kuanza kazi kwa chombo hicho. Pamoja na hilo, litatunga sheria ambazo zitaiweka Libya kwenye uchaguzi kamili wa bunge baada ya kuandikwa kwa katiba mpya hapo mwakani.
Ulinzi uliimarishwa vikali kwenye tukio hilo lililodumu kwa dakika 40 kutokana na machafuko yanayoendelea mjini Tripoli na huko Benghazi ambako kumetokea mripuko garini siku ya Jumamosi katika eneo la soko.
Wawakilishi wa makundi ya kijamii, mabalozi mbalimbali waliomo nchini humo, pamoja na viongozi wa ngazi za juu wa NTC wamehudhuria sherehe hizo.
Muda mfupi baada ya tukio hilo, nderemo na vifijo vilisikika kwenye mitaa ya mji mkuu wa Tripoli huku mabaluni yakirushwa angani. Raia nchini humo wamesikika wakisema kuwa "Libya itakuwa nchi huru na yenye demokrasia siku zote".
Lakini kando ya furaha hiyo bado raia hao wanahofu na hali ya usalama kutokana na baadhi ya makundi kugoma kuweka silaha chini. Naibu Waziri Mkuu Mustafa Abu Shagour aliambia Shirika la habari la Reuters kwamba suala la kudhibiti hali ya usalama ndiyo kipaumbele cha nchi ambacho utawala wowote utakaokuja madarakani lazima uzingatie.
Mwandishi: Stumai George/Reuters/AFP
Mhariri: Sekione Kitojo