Mzozo wa Mashariki ya Kati wasababisha kitisho kikubwa cha nishati
19 Novemba 2026
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kimataifa la Nishati IEA, Fatih Birol, ameandika katika ripoti ya kila mwaka ya shirika hilo kuhusu mtazamo wa nishati duniani iliyotolewa leo kwamba mgogoro katika mlango bahari wa Hormuz umesababisha tishio kubwa zaidi kwa usalama wa nishati katika historia, tishio ambalo ni kubwa zaidi kuliko misukosuko ya mafuta iliyotokea katika miaka ya 1970.
Katika utangulizi wake wa ripoti hiyo, Birol alielezea juhudi zilizochukuliwa na nchi mbalimbali ili kuzilinda kaya, huku nchi zinazosafirisha mafuta zikiongeza usambazaji katika soko na kutumia njia mbadala, huku China ikipunguza kiasi cha mafuta inayonunua kutoka katika masoko ya kimataifa.
Birol aidha amesema serikali zimeingilia kati ili kujaribu kuwapa walaji kinga fulani, lakini bado wanakabiliwa na bei za juu na katika baadhi ya matukio, uhaba wa bidhaa.
Katika ripoti yake hiyo kuu ya kila mwaka, shirika la kimataifa la nishati limesema mzigo unazidi kuangukia kwa watumiaji na walaji, huku dunia ikikosa njia nyingine za kukabiliana na athari za mgogoro huo kwenye usambazaji wa nishati.
Shirika hilo limeonya kwamba mgogoro huo wa mashariki ya kati hasa katika mlango bahari wa Hormuz, kama ilivyokuwa kwa misukosuko ya nishati ya hapo awali, bila shaka utawacha alama za kudumu.
Korea Kaskazini yatanua kinu chake cha Yongbyon
Wakati haya yakiarifiwa, mkurugenzi mkuu wa shirika la kimataifa la nishati ya atomiki IAEA, Rafael Grossi, amesema Korea Kaskazini imekuwa ikitanua kituo chake cha awali cha kurutubisha urani katika kinu chake kikuu cha nyuklia cha Yongbyon. Hii ni ishara nyingine inayoonyesha kuwa Korea Kaskazini inatekeleza ahadi yake ya kuimarisha mpango wake wa silaha za nyuklia.
Grossi alisema katika taarifa yake kwa Bodi ya Magavana ya IAEA siku ya Jumatano kwamba tangu katikati ya Septemba 2026, upanuzi zaidi wa kituo cha awali cha kurutubisha urani huko Yongbyon umekuwa ukiendelea, huku sehemu hiyo mpya ikiwa imekamilika kwa nje kufikia mwishoni mwa Oktoba 2026. Grossi alisema utanuzi unaoendelea wa mpango wa Korea Kaskazini wa kurutubisha urani bado ni jambo linalotia wasiwasi mkubwa.
Shirika la IAEA laelezea matumaini kuhusu Iran
Kuhusu Iran, Grossi alisisitiza tena imani yake kwamba kupitia hatua za taratibu, na kwa kusikiliza hoja zozote zinazoweza kuwepo kuhusiana na usalama, wanaweza kupiga hatua katika kutafuta makubaliano kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.
"Hali ni mbaya. Tunawaalika na kuwasihi marafiki zetu wa Iran kurejea katika ushirikiano nasi. Tunafahamu pia kuwa kuna mashauriano muhimu ya kidiplomasia ambayo yatahitaji, bila shaka, msingi wa uthibitishaji ambao unaweza kupatikana pekee kupitia kazi ya Wakala. Wakala uko tayari. Naamini tunapaswa kutoa mchango huu ili kuhakikisha kuwa amani inatawala, na kwamba matumizi ya nishati ya nyuklia kwa madhumuni ya amani yanaweza kuendelea nchini Iran na kote duniani.”
Kuhusu Ukraine, Grossi alisema hali hiyo inaendelea kuwa chanzo cha wasiwasi mkubwa. Alisema wamekuwa wakizingatia kuhakikisha kuwa utulivu dhaifu uliopo, kwa kuzingatia usalama wa nyuklia pekee katika kinu cha kuzalisha nishati ya nyuklia cha Zaporizhzhya, unadumishwa. Na hili linafanyika kupitia makubaliano kadhaa ya kusitisha mapigano ambayo wameyafanyia mazungumzo.