1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nyaraka za Pandora: Wanasiasa wakubwa watajwa kukwepa kodi

4 Oktoba 2021

Nyaraka za Pandora zimebainisha kuwa viongozi wapatao 35 ulimwenguni kote na mabilionea kadhaa wanamiliki kampuni au akaunti za benki za nje kukwepa kulipa kodi.

Symbolbild | Pandora Papers
Picha: ICIJ

Akaunti za benki zinazofunguliwa nje ya nchi mara nyingi hutumiwa ili kuhamisha pesa nyingi kisiri na kuficha utajiri wa kweli wa mtu.

Uchunguzi huo uliofanywa na Jumuiya ya Kimataifa ya Wanahabari wa Upelelezi (ICIJ) na timu ya vituo 150 vya habari - pamoja na idhaa ya Kituruki ya DW - umegundua kuwa watu mashuhuri wapatao 330 ulimwenguni kote wanamiliki akaunti kama hizo za siri za nje ya nchi.

Mawaziri wa fedha wa Pakistan, Uholanzi na Brazil na mawaziri wa zamani wa fedha wa Malta na Ufaransa - pamoja na mkuu wa zamani wa Shirika la Fedha Dominique Strauss-Kahn, wote wanakwepa kodi kwa kupitia makampuni yaliyowekeza nje ya nchi.

Soma zaidi: Infantino azungumzia Nyaraka za Panama

Kulingana na uchunguzi huo wa ICIJ, Nyaraka za Pandora zinaonyesha kuwa watu wenye vyeo vya ngazi za juu ambao wangeweza kusaidia kukomesha mfumo huo wa kukwepa kodi badala yake wananufaika nao. Kwa kutumia mfumo huo wanahamisha mali kwenye kampuni za siri na huku serikali zikishindwa kupunguza kasi ya mtiririko wa pesa haramu ulimwenguni ambao unatajirisha wahalifu na kuongeza umaskini katika mataifa duni. 

"Tunaangalia mfumo ambao unadhuru watu, unaudhuru ulimwengu. Na ni muhimu kwa watu kuufahamu," amesema Gerard Ryle, mkurugenzi wa ICIJ.

Waziri wa Mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Blair ambae kwa miongo kadhaa amekuwa mstari wa mbele kukemea mtindo huo wa kukwepa kodi,  pamoja na mke wake wametajwa katika nyaraka hizo kuwa waliweza kumiliki jengo lenye thamani ya euro milioni 7.6 wakati waliponunua kampuni inayowekeza nje ya nchi kutoka kwa familia ya waziri wa utalii wa Bahrain, Zared bin Rashid al-Zayani. Kwa kununua hisa za kampuni hiyo - na sio nyumba yenyewe-  Blair na mkewe Cherie walikwepa kulipa kodi ya nyumba ya takriban dola 400,000.

Tony Blair, waziri mkuu wa zamani wa UingerezaPicha: Dan Kitwood/Getty Images

Waziri Mkuu wa Czech Andrej Babis, bilionea ambaye aliingia madarakani mnamo 2017 na ahadi ya kukabiliana na ufisadi, pia ametajwa katika Nyaraka za Pandora. Babis hakutoa kauli yoyote hadi sasa kwa waandishi habari.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy pia ametajwa kuwa anamiliki hisa katika kampuni iliyosajiliwa katika Visiwa vya Virgin vya Uingereza.

Naye Mfalme Abdullah II wa Jordan ametajwa kuwa mnamo mwaka 2011 alinunua majumba matatu ya ufukweni mwa bahari kwa jumla ya dola milioni 68 Malibu kupitia kampuni hizo zinazowekeza nje ya nchi, katika wakati ambapo raia wa  Jordan wakiandamana kupinga ufisadi na ukosefu wa ajira nchini humo.

Kwa upande wa Afrika, Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na mama yake wametajwa kwenye nyaraka hizo kuwa wanamiliki akaunti za siri Panama. Aidha, ndugu zake watatu, wanamiliki kampuni tano za nje ya nchi  zenye thamani ya zaidi ya dola milioni 30. Kenyatta na familia yake hawakujibu maombi ya ICIJ ya kutoa maoni yao juu ya taarifa hizo.

Soma zaidi: Wanasiasa wakubwa watajwa katika kashifa ya ukwepaji kodi ya "Paradise Papers"

Nyaraka za Pandora zimedhihirishwa miaka mitano baada ya uchunguzi wa kihistoria wa Nyaraka za Panama, ulioutikisa ulimwengu mnamo mwaka 2016. Uchunguzi huo ulisababisha wabunge katika mataifa kadhaa kupitisha sheria mpya, na wanasiasa kadhaa wa ngazi za juu kujiuzulu – ikiwa ni pamoja na mawaziri wakuu wa Iceland na Pakistan.

Chanzo: dw

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW