Nyongeza ya muda wa kusitisha mapigano yaheshimiwa Kongo
19 Julai 2024Hali hiyo imeshuhudiwa, siku moja baada ya Marekani kutangaza kwamba pande hizo za majeshi ya serikali na waasi wa M23, zimekubaliana kuongeza muda wa kusimamisha mapigano kwa siku 15.
Makubaliano hayo ya kusitisha mapigano yalianza mnamo Julai 5 na yataendelea hadi Julai 19, limeserma Baraza la Usalama la Kitaifa katika ikulu ya Marekani.
Kwa upande wake msemaji wa jeshi la Kongo luteni Mbuyi Reagan, amelithibitishia shirika la habari la AFP kwamba hali ya utulivu inaendelea katika eneo hilo.
Hata hivyo rais wa Mtandao wa Amani wa Kongo, Patrick Kikandi amesema hata kama mapigano kati ya waasi na majeshi ya serikali yamepungua tangu kuanza kwa makubaliano hayo lakini pande zote ziko katika harakati za kujiandaa kuanzisha tena vita.
Waasi wa M23, wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda, walianzisha mashambulizi katika jimbo la Kivu Kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mwishoni mwa mwaka 2021 na tangu wakati huo wamedhibiti eneo kubwa la ardhi katika jimbo la Kivu kaskazini.