1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Sanaa

Nyota wa Bollywood Salman Khan atoka jela kwa dhamana

7 Aprili 2018

Nyota wa filamu wa Bollywood Salman Khan ameondoka gerezani baada ya kupewa dhamana ili apinge hukumu ya kifungo cha miaka mitano kwa kuuwa swala adimu miongo miwili iliopita.Khan anasema alibambikiziwa kesi.

Indien Salman Khan auf dem Weg zum Gericht
Picha: picture-alliance/AP Photo/S. Verma

Mamia ya mashabiki walimsubiri nyota huyo mwenye umri wa miaka 52 wakati gari lake likipita kwa kasi katika milango ya jela kuu ya Jodhpur, ambako nyota huyo wa filamu za mapigano alifungwa kwa siku mbili baada ya kuhukumiwa siku ya Alhamisi.

Baadhi walijaribu kudandia pembeni mwa gari hilo lakifahari na pikipiki kadhaa zilimfuata Khan wakati akiendeshwa kwa kasi kuelekea uwanja wa ndege wa Jodhpur ambako ndege ya kukodi ilikuwa ikimsubiri.

Makundi ya watu -- wakiwemo wanaume wengi wanaoiga mitindo wa Khan ya nywele na mavazi -- pia yalikusanyika nje ya nyumba yake ya kifahari mjini Mumbai, wakicheza baadhi ya nyimbo zilizomo kwenye filamu zake.

Jaji alimkubalia Khan, mmoja wa waigizaji wanaolipwa fedha nyingi zaidi duniani, dhamana ya rupee 50,000 (Dola 770). Hawezi kuondoka India bila kibali cha mahakama.

Khan hakuhudhuria kikao cha kusikiliza maombi yake ya dhamana lakini mwendesha mashtaka Mahipal Bishnoi alismea muingizaji huyo anapaswa kufika mahakamani Mei 7.

Kundi kubwa la mashabiki wa Khan na wadau wa Bollywood, walishangazwa na hukumu ya awali katika mji wa jimbo la Rajasthan katika kesi hiyo ya miaka 20.

Watu wa jamii ya Bishnoi wakisherehekea baaday a Salman Khan kuhukumiwa kifungo cha miaka 25 gerezani.Picha: Reuters/Stringer

Khan alikanusha kuwapiga risasi na kuwauwa swala wawili adimu wanaofahamika kama "black bucks" wakati wa safari yake ya uwindaji alipokuwa akitengeneza filamu mwaka 1998. Lakini wakati mashabiki wake na watengenezaji wa filamu zijazo wanaweza kupata ahueni, Khan bado anakabiliwa mshikemshike mahakamani.

Shirika la haki za wanyama la PETA, lilisema limevunjwa moyo na dhamana ya Khan. "Wakati Salman Khan kwa sasa anarudi nyumbani kuishi maisha yake kama nyota wa filamu, "black bucks" walilipa gharama kubwa, kwa maisha yao," alisema Manilal Valliyate, Afisa mtendaji Mkuu wa PETA India katika taarifa.

Khan ameituhumu idara ya misitu ya Rajasthana kwa kujaribu kumbambikizia kesi. Mawakili wake wanadai swala hao wa "black buck" walikufa kutokana na sababu za kiasili kama vile joto kali, na kusisitiza kuwa hakukuwa na ushahidi kwamba walipigwa risasi.

Nyota wengine wanne wa Bollywood -- Saif Ali Khan, Sonali Bendre, Tabu na Neelam Kothari -- ambao pia walituhumiwa katika kesi hiyo waliachiwa kutokana na ukosefu wa ushahidi.

Khan anaendelea kuwa nyota mkali wa Bollywood licha ya sakata hilo, akishiriki katika filamu zaidi ya 100 na vipindi vya televisheni. Alimaliza wa pili nyuma ya Sha Rukh Khan mwaka 2017 katika orodha ya waigizaji wanaolipwa zaidi Bollywood. Khan hao wawili ni miongoni mwa waigizaji wanaolipwa fedha nyingi zaidi duniani.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe.

Mhariri. Yusra Buwayhidi

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW