1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nyumba na biashara milioni 3 zaachwa bila umeme Florida

10 Oktoba 2024

Kimbunga Milton kimepiga jimbo la Florida nchini Marekani na kusababisha uharibifu mkubwa kote katika eneo la katikati mwa jimbo hilo pamoja na kuacha zaidi ya nyumba na biashara milioni 3 bila umeme kufikia mapema leo.

Kimbunga Milton chapiga jimbo la Florida nchini Marekani Oktoba 9, 2024
Kimbunga Milton chapiga jimbo la Florida nchini MarekaniPicha: CHANDAN KHANNA/AFP

Kimbunga Milton kilipiga jimbo la Florida kikiwa na nguvu za kiwango cha tatu kwenye kipimo kinachopima ukubwa wa vimbunga, na kusababisha hasara kubwa kwenye pwani ambayo bado ilikuwa inakabiliwa na athari za Kimbunga Hellen.

Kimbunga Milton kilisababisha upepo wenye kasi ya zaidi ya maili 100 kwa saa lakini kilikosa kupiga moja kwa moja mji wa Tampa.

Dhoruba hiyo ilielekea kusini katika masaa ya mwisho usiku wa jana, ikapiga mji wa Siesta Key, karibu na Sarasota, umbali wa maili 70 kusini mwa Tampa.

Hali katika mji wa Tampa bado ni ya dharura

Hali katika eneo la Tampa bado ilikuwa ya dharura, huku St. Petersburg ikipata mvua zaidi ya inchi 16, na Huduma ya Kitaifa ya Hali ya Hewa ikionya juu ya mvua kubwa katika maeneo ya kusini na katikati mwa Florida.

Jimbo la Florida lakabiliwa na hatari ya kimbunga Milton

Uwanja wa Tropicana, ambao ni nyumbani kwa timu ya besiboli ya Tampa Bay Rays huko St. Petersburg, ulishuhudia uharibifu mkubwa, kwani kitambaa cha paa lake kiliraruliwa na upepo. Mashine nyingi za kubeba mizigo mizito pia ziliharibiwa.

Robin Haight mkazi wa Fort Myers, Florida apelekwa hospitalini baada ya kujeruhiwa wakati upepo mkali ulipopiga nyumba yakePicha: CHANDAN KHANNA/AFP

Wakazi wa St. Petersburg walipoteza huduma ya maji kutokana na kupasuka kwa bomba kuu la maji, ambalo lilisababisha kukatizwa kwa huduma hiyo.

Kimbunga Milton sio cha kwanza Florida

Hata kabla ya Kimbunga Milton, vimbunga vingine vilikuwa vimepiga Florida. Klabu ya The Spanish Lakes karibu na Fort Pierce, kwenye Pwani ya Atlantic ya Florida, ilipata athari kubwa, nyumba zikiharibiwa na baadhi ya wakazi kuuawa.

Biden kuyatembelea maeneo yaliyoathiriwa na kimbunga Helene

Afisa mkuu wa Kaunti ya St. Lucie, Keith Pearson, aliiambia kituo cha habari WPBF kuwa watu kadhaa walifariki, ingawa hakutoa idadi kamili ya vifo.

Kulingana na Kevin Guthrie, mkurugenzi wa kitengo cha usimamizi wa hali za dharura jimboni Florida, takriban nyumba 125 ziliharibiwa kabla ya kimbunga hicho kufika ufukweni, nyingi kati yao zikiwa nyumba za muda katika jamii za wazee.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW