1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UfisadiKimataifa

Saa za Rolex zamuingiza matatani Rais wa Peru

30 Machi 2024

Maafisa nchini Peru wamevamia nyumba ya Rais Dina Boluarte siku ya Jumamosi kama sehemu ya uchunguzi unaoendelea wa ufisadi unaohusiana na saa za kifahari za Rolex ambazo hakuzitaja, hatua iliyolaaniwa vikali na serikali

Peru | Rais Dina Boluarte
Rais Dina Boluarte anatuhumiwa kujikusanyia saa kadhaa za kifahari za Rolex bila kuzitangaza.Picha: Guadalupe Pardo/AP Photo/picture alliance

Kulingana na waraka wa polisi ambao shirika la habari la AFP limepata nakala yake, takriban maafisa 40 walihusika katika uvamizi huo, ambao ulikuwa unatafuta saa za kifahari aina ya Rolex ambazo Boluarte hakuwa amezitangaza hadharani. Polisi imesmea uvamizi huo ulikuwa wa kufanya upekuzi na kukamata.

Rais huyo anaekabiliwa na misukosuko hakuonekana kuwa nyumbani wakati huo. Waziri Mkuu Gustavo Adrianzen alilaani uvamizi huo akisema ni "ghadhabu isiyovumilika" na "iliovuka mipaka na ni kinyume cha katiba."

Maafisa walianzisha uchunguzi dhidi ya Boluarte mwezi huu baada ya chombo cha habari kuangazia picha za saa zake za kifahari za michezo kwenye hafla za umma. Uvamizi wa Jumamosi, ambao ulikuwa operesheni ya pamoja kati ya polisi na ofisi ya mwendesha mashtaka, ulitangazwa kwenye kituo cha runinga cha Latina.

Polisi wakiwa nje ya nyumba ya Rais Dina Boluarte wakati wa uvamizi ulioamriwa na ofisi ya mwendesha mashtaka mkuu, ukilenga kukamata saa za Rolex kama sehemu ya uchunguzi wa awali juu ya madai ya kujitajirisha kinyume cha sheria mjini Lima, Peru, Jumamosi, Machi 30, 2024.Picha: Martin Mejia/AP Photo/picture alliance

Maafisa wa serikali walionekana wakiizunguka nyumba hiyo katika Wilaya ya Surquillo ya mji mkuu Lima huku maafisa wakizuia magari yanayokuja. Uvamizi huo wa kushtukiza, wa asubuhi na mapema uliombwa na mwendesha mashtaka wa umma na kuidhinishwa na Mahakama Kuu ya Upelelezi wa Awali.

Kadhia hiyo yaongezea madhila ya Rais Boluarte

Akiwa tayari anakabiliwa na kushuka kwa viwango vya umaarufu wake, Boluarte ametumbukia katika mzozo mpya wa kisiasa kwa kuanzishwa uchunguzi wa iwapo amejitajirisha kinyume cha sheria akiwa madarakani.

Soma pia: Wabunge wa Peru wawasilisha ombi la kumng'oa rais Boluarte

Iwapo atakutwa na kesi ya kujibu, mashtaka dhidi yake hayataweza kuendeshwa hadi baada ya muhula wake kukamilika Julai 2026 au aondolewe madarakani, kwa mujibu wa katiba.

Makumi ya waandishi wa habari walifika nyumbani kwa rais huyo siku ya Jumamosi lakini waendesha mashtaka na maafisa katika eneo la tukio hawakujibu maswali. Ofisi ya rais wa Peru pia haikujibu mara moja. 

Kashfa hiyo iliibuka baada ya chombo cha habari cha "La Encerrona" kuripoti katikati mwa mwezi Machi kwamba Boluarte alikuwa amevaa saa mbalimbali za Rolex kwenye hafla rasmi. Chombo hicho kiliangazia saa hizo kwa kuchapisha picha za kuanzia Desemba 2022, wakati Boluarte alipochukua madaraka. 

Polisi na waendesha mashtaka wakisimama nje ya nyumba ya Rais Dina Boluarte wakati wa uvamizi uliokusudiwa kukamata saa aina ya Rolex, kama sehemu ya uchunguzi wa ufisadi dhidi ya rais huyo.Picha: Martin Mejia/AP Photo/picture alliance

Baadae mamlaka ya udhibiti wa serikali ilitangaza kuwa ingepitia matamko ya mali ya Boluarte kutoka miaka miwili iliyopita ili kutafuta kasoro zozote. Boluarte, 61, amejitetea kwa nguvu. "Niliingia Kasri la Serikali nikiwa na mikono misafi, na nitaliacha nikiwa na mikono misafi," alisema wiki iliyopita.

Soma pia: Bunge la Peru lamwapisha Rais mpya Dina Boluarte

Akijibu maswali kuhusu jinsi alivyoweza kumudu saa za bei ghali kwa mshahara wa umma, alisema saa hizo ni zao la kufanya kazi kwa bidii tangu alipokuwa na umri wa miaka 18.

Wakili huyo na makamu wa rais wa zamani aligeuka rais wa kwanza mwanamke wa Peru baada ya kiongozi wa mrengo wa kushoto Pedro Castillo kujaribu kulivunja Bunge na kutawala kwa amri, na kupelekea kuondolewa kwake haraka na kukamatwa.

Maandamano makali ya kumtaka Boluarte ajiuzulu na uchaguzi mpya ufanyike yalifuatia, huku takriban watu 50 wakiuawa katika msako mkali uliofuata.

Chanzo: AFPE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW