Obama aahidi maendeleo
7 Novemba 2012Baada ya kupata fursa ya kuhutubia umma rais Obama alisema kwamba uchaguzi huo wa watu wa Marekani unawakumubusha kwamba wakati barabara yao imekuwa ngumu na safari yao pia imekuwa ndefu, tayari wapo safarini, wametafuta njia na kwamba wanatambua kutoka moyoni mwao kwamba wanajukumu kubwa na kuahidi kwamba mambo mazuri yanakuja.
"Ninaamini tunaweza kutimiza misingi ya ahadi tuliyo nayo, la msingi ni kwamba kama unataka kufanya kazi sana haijalishi wewe ni nani,au unatokea wapi, au unaonekanaje au wapi unapenda. Haijalishi wewe ni mweusi au mweupe, au Muhispania au Muasia, au Mmarekani asilia, au kijana au mzee, au tajiri au masikini, mlemavu au mkamilifu, shoga au mtu wa kawaida unaweza kuleta ushindi Marekani kama unataka kujaribu". Rais Obama alisema maeneo hayo ya kutia faraja mbele ya umati mkubwa wa wamarekani akiwa katika mji wake wa nyumbani huko Chicago.
Obama aahidi kushirikiana na Republican
Akiwa jukwaani na mke wake na watoto wake Sasha na Maria alirejelea maneno ya kupigania maisha bora kwa watu wa kipato cha wastani na kutimiza ndoto ya kuifanya Marekani kuwa taifa lenye tija zaidi. Aidha alisisitiza kwamba katika kutimiza azma hiyo na hasa kupunguza nakisi,kuleta mabadiliko katika sheria za uhamiaji na kupunguza hali ya taifa hilo kutegemea mafuta kutoka nje amesema watashirikiana na viongozi wa Republican pia.
Romney ampongeza Obama
Kwa upande wake Romney aliwaambia wafuasi wake kwamba alikuwa akisali wakati wote ili aweze kushinda nafasi ya urais wa taifa hilo kubwa kabisa duniani. Akizungumza kabla ya kuungana na mkewe Ann, sambamba na familia yake na mgombea mwenza Paul Ryan alisema vilevile angalipenda kutimiza matakwa yao ya kuliongoza taifa hilo katika mwelekeo mpya lakini taifa limechagua kiongozi mwingine. Kwa hivyo yeye, mke wake pamoja na wafuasi hao wanaungana kumuombea heri rais Obama na taifa hilo kubwa kwa ujumla.
Obama anachaguliwa tena kuongeza taifa hilo kwa kipindi kingine cha miaka menne wakati taifa hilo likikabiliwa na kiwango kikubwa cha tatizo la ajira la asilimia 7.9. Kumbukumbu zonaonesha hakuna rais wa Marekani aliengia madarakani kwa awamu ya pili tangu kumalizika kwa vita vya pili vya dunia kukiwa na kiwango cha tatizo la ajira cha asilimia 7.2. Ukuaji wa kiwango cha ajira kwa mwaka huu 2012 kimesalia asilimia mbili. Lakini kwa wakati wote rais Obama alikuwa akiwakumbusha wapiga kura kwamba hali hiyo amerithi baada ya kuchaguliwa kwake 2008.
Mwandishi: Sudi Mnette/RTR/DPA
Mhariri:Yusuf Saumu