Obama aamini Congress itakubali vita vya Syria
3 Septemba 2013Rais Barack Obama ameelezea matumaini yake kwamba Congress itaupitisha mpango wake wa kuingilia kati kijeshi nchini Syria hayo baada ya kukutana na viongozi wa Congress, akiongeza kwamba Marekani ina mpango mkubwa zaidi wa kuwasaidia waasi kuvishinda vikosi vya Rais Bashar al-Assad.
Katika mkutano huo uliofanyika kwenye Ikulu ya White House, Obama ametoa wito kwa bunge kuupigia kura ya ndio mpango huu, akirejelea kwamba ni mpango wenye mipaka maalum na hautakuwa marejeo ya vita virefu vya Iraq na Afghanistan.
"Tunachokilenga ni kitu cha muda mfupi. Ni jambo ambao litapunguza uwezo wa Assad. Lakini wakati huo huo tuna mkakati mkubwa zaidi ambao utatuwezesha kuinua uwezo wa upinzani." Amesema Rais Obama.
Mtaalamu wa kemikali wa Syria akimbilia Istanbul
Katika hatua nyengine, mtaalamu wa kemikali wa serikali ya Assad, Abdeltawwab Shahrour, anayesemekana kuwa na ushahidi unaothibitisha kwamba serikali ilitumia silaha za kemikali kwenye mashambulizi yake karibu na mji wa Aleppo mnamo mwezi Machi, amekimbia Istanbul, Uturuki.
Sharour aliyekuwa mkuu wa kamati ya madawa ya mji wa Aleppo, alitarajiwa kujitokeza hadharani leo kuonesha ushahidi kwamba vikosi vya Assad vilikishambulia kiunga cha Khan al-Assal, tarehe 19 Machi, kwa kutumia silaha hizo za kemikali.
Kwa mujibu wa msemaji wa makundi ya upinzani yenye makao yake mjini Istanbul, miongoni mwa ushahidi alionao Shahrour ni nyaraka na ushahidi wa wazi kutoka kwa viongozi wa polisi ambao unakinzana na kile kilichosemwa na serikali ya Assad juu ya mashambulizi hayo yaliyouwa zaidi ya watu 20.
Ikiwa ushahidi huo utakuwa na uzito, basi huenda ukaongezea uzito hoja ya utawala wa Rais Barack Obama wa Marekani ya kuivamia Syria kijeshi, kutokana na tuhuma za utawala wa Assad kutumia silaha za sumu.
Congress huenda ikamkubalia Obama
Hivi leo bunge la nchi hiyo, Congress, linafanya kikao chake cha kwanza juu ya mipango hiyo ya kijeshi, ambapo utawala wa Obama unajaribu kuwashawishi wabunge na Wamarekani wenye mashaka na hoja hiyo ya kujibu mashambulizi mengine ya kemikali yanayoshukiwa kufanywa na vikosi vya Assad, kando kidogo ya mji mkuu, Damascus, mwezi uliopita.
Waziri wa Mambo ya Nje John Kerry, mwenzake wa Ulinzi Chuck Hagel na mkuu wa majeshi, Jenerali Martin Dempsey walitarajiwa kukutana na Kamati ya Mambo ya Nje ya Baraza la Seneti hivi leo. Ikulu ya Marekani inasema ina ushahidi wa kutosha kuthibitisha kwamba wanajeshi wa Assad walitumia silaha za kemikali.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Seneta Robert Menendez, amesema anaamini jopo lake linaweza kumuunga mkono Rais Obama, lau ataweza kuelezea kwa undani wa matumizi ya nguvu dhidi ya Syria yatakavyokuwa na pia matokeo yake.
Hata hivyo, baada ya muongo mzima wa vita nchini Iraq na Afghanistan, kura za maoni zinaonesha kwamba Wamarekani wengi wanapinga hatua yoyote ya kijeshi nje ya mipaka ya nchi yao.
Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Saumu Yusuf