1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama afanya ziara ya mwisho Ulaya

Isaac Gamba
15 Novemba 2016

Rais wa Marekani Barack Obama yuko Athens, Ugiriki moja ya nchi anazozitembelea katika ziara yake ya mwisho ya kigeni kabla ya kuondoka madarakani


US Präsident Barack Obama PK
Picha: Picture-Alliance/AP Photo/S. Walsh

Ushindi wa Donald Trump dhidi ya mgombea wa chama cha Democrat Hillary Clinton unaelekea kubadilisha mtizamo wa awali wa ziara hiyo ya Rais 44 wa Marekani Barack Obama anayeondoka madarakani mwezi Januari, hasa kuhusiana na makubaliano ya mikataba kadhaa ya kimataifa ikiwa ni pamoja na makubaliano yaliyofikiwa kuhusiana na mpango wa nyukilia wa Iran na wa mazingira.

Wakati wa kikao chake na waandishi wa habari hapo jana mjini Washington, Rais Obama alijaribu kuwahakikishia washirika wa Marekani walio na mashaka kuwa haitakuwa rahisi kubadilisha au kuvunja mikataba hiyo.

Mara  baada ya kuwasili mjini Athens mnamo wakati ulinzi ukiwa umeimarishwa zaidi, Rais Obama alitarajiwa kuwa  na kikao cha pamoja na waandishi wa habari na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Alexis Tsipras.

Obama atakutana na Merkel nchini UjerumaniPicha: Picture-alliance/AP Photo/M. Sohn

Suala la mzigo wa madeni unaoikabili Ugiriki pamoja na kusuasua kwa uchumi kutokana na mgogoro wa kiuchumi unaoikumba nchi hiyo, linatarajiwa kupewa uzito wa juu katika ziara hiyo ya kwanza ya Rais Obama nchini humo.

Baada ya ziara yake nchini Ugiriki, Rais Obama anatarajiwa kuelekea nchini Ujerumani ambako atakutana na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, na baadaye kwenda nchini Ufaransa ambako atafanya mazungumzo na Rais wa nchi hiyo Francois Hollande kabla ya kwenda Uingereza na  Italia ambako pia atakuwa na mazungumzo na viongozi wa nchi hizo.

Rais Barack Obama atakamilisha ziara yake hiyo kwa kuzuru Peru katika mkutano wa kilele wa ushirikiano wa kiuchumi wa nchi za Asia na Pacific (APEC) ambako miongoni mwa viongozi anaotarajiwa kufanya nao mazungumzo ni Rais wa China Xi Jinping.

Akizungumza hapo jana na waandishi wa habari kabla ya kuondoka nchini mwake, Rais Obama alikiri kuwa na mashaka na mrithi wake katika nafasi hiyo na ujumbe alioutoa jana ulionyesha kuwa faraja kwa wale wote ambao bado wana wasiwasi kufuatia ushindi huo wa Trump na ambalo pia linaonekana kuwa somo la kipekee kwa Rais huyo ambaye sasa atakuwa Rais wa 45 wa Marekani.  Akifafanua zaidi Obama alisema.

Mustakabali wa mahusiano ya Marekani na Ulaya utajadiliwaPicha: picture-alliance/dpa

OTON . Katika mazungumzo yangu na Rais Mteule, alielezea juu ya nia yake ya dhati  ya kuendeleza uhusiano wa kimkakati na kuwa moja ya ujumbe ambao nitaweza kuuwasilisha  ni juu ya hatua yake ya kuzingatia umuhimu wa ushirikiano wa Marekani katika jumuiya ya NATO pamoja na uhusiano wa Marekani na nchi za ulaya na nadhani hilo ndilo jukumu ambalo pia nitalitilia mkazo wakati wa ziara yangu na nataka wafahamu kuwa uhusiano na jumuiya kama vile NATO  si muhimu tu kwa ulaya bali  pia kwa Marekani na dunia kwa ujumla.

Bilionea Donald Trump ambaye hajawahi kushika nafasi yoyote ya kisiasa alikuwa tayari ameahidi katika mikutano yake ya kampeni kufanya mabadiliko katika baadhi ya nyanja muhimu za mahusiano kimataifa kuhusu nchi hiyo.  Hata hivyo Rais Obama  alisema suala la kuwafukuza mamilioni ya wahamiaji wanaoishi nchini Marekani pamoja na suala la makubaliano ya mkataba wa nyukilia wa Iran  na masuala yanayayohusu mazingira  si masuala ambayo  yanaweza kufanyiwa uamuzi kirahisi. 

Aidha Obama amesema katika mazungumzo yake na Trump alimueleza kuwa kauli  na maamuzi yake yanaweza kuleta athari katika masoko, kusababisha vita pamoja na kubadilisha pia mtizamo wa watu ambapo pia alimueleza kuwa katika uchaguzi wa aina ile wa Marekani ambao  ulikuwa na ushindani pamoja na mgawanyiko mkubwa, ni muhimu kutoa kauli zinazoonyesha kujenga mshikamano na umoja miongoni mwa jamii.

Mwandishi: Isaac Gamba/ AFPE
Mhariri : Caro Robi

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW