Obama afupisha kifungo cha mvujisha siri za Marekani
18 Januari 2017Afisa wa ikulu ya Marekani amesema kufipishwa kifungo hicho hakuhusiani na hatua ya sasa ya Marekani ya kuhusishwa tena mtandao wa WikiLeaks katika uchaguzi wa Marekani wa mwaka jana ama ahadi ya muasisi wa mtandao huo Julian Assange ya kukubali kupelekwa Marekani iwapo Manning angeachiwa huru.
Manning aliibua mjadala mkubwa kimataifa kutokana na kitendo chake cha kuvujisha siri za serikali kwa mtandao wa WikiLeaks akitoa nyaraka 700,000 za siri , mikanda ya vidio ya taarifa za serikali na taarifa za siri za kivita hali iliyopelekea ahukumiwe kifungo cha miaka 35 gerezani.
Rais Barack Obama katika moja ya hatua zake za hivi karibuni kabla ya kuondoka madarakani ameamua kufupisha kifungo cha Manning hadi miaka saba hatua ambayo imeonekana kuwakasilisha warepublican.
Spika wa bunge la wawakilishi Paul Ryan katika taarifa yake amelaumu uamuzi huo akisema ni hatari hasa kuhusiana na kuwapa nafuu wale ambao wanavujisha taarifa nyeti za serikali.
Manning alikuwa akifanya kazi kama mchambuzi wa masuala ya kijasusi mjini Baghdad mnamo mwaka 2010 wakati alipovujisha taarifa za siri za kivita ikiwa ni pamoja na mkanda wa vidio ulionyesha helikopta ya kivita ya Marekani ikishambulia washukiwa wa uasi dhidi ya serikali ya Iraq ambapo watu kadhaa waliuawa wakiwemo waandishi wa habari wawili wa shirika la habari la Reuters.
Seneta wa Republican Tom Cotton amesema kuvujishwa kwa taarifa hizo za siri zilileta hatari kubwa kwa wanajeshi wa Marekani, maafisa wa kijasusi, wanadiplomasia pamoja na washirika wao.
Manning aishi kama mwanamke wa jinsia mbili
Manning alizaliwa kama mwanaume lakini baada ya kutiwa hatiani alijitambulisha kuwa ni mwanamke. Ikulu ya White House imesema kifungo chake kitafikia mwisho May 17 mwaka huu.
Manning ambaye amekuwa akipambana kuishi kama mwanamke mwenye jinsia mbili na huku pia akijaribu mara mbili kutaka kujiua katika gereza la wanaume la Fort Leavenworth, Kansas alikubali kuvujisha taarifa hizo za siri hatua ambayo inaelezwa kuchangia uamuzi wa Rais Barack Obama wa kufupisha kifungo chake.
Mmoja wa maafisa wa Ikulu ya Marekani ambaye hakutaka kutajwa jina amesema uamuzi huo wa Obama umezingatia kifungo cha Manning kuwa kirefu zaidi ukilinganisha na vifungo vinavyotolewa kwa watu wengine waliofanya uhalifu wa aina hiyo.
Hata hivyo Ikulu imesema uamuzi huo wa Rais Obama hauhusiani na hatua ya sasa ya WikiLeaks ambapo imekuwa ikihusishwa na kuchapisha barua pepe wiki chache kabla ya uchaguzi wa Novemba 8, mwaka jana hatua ambayo mashirika ya kijasusi ya Marekani yanaamini kuwa ilichangia pia Urusi kuingilia uchaguzi huo kwa lengo la kushawishi matokeo ya uchaguzi huo.
Rais Obama ambaye ataondoka rasimi madarakani Ijumaa wiki hii atafanya mkutano wake wa mwisho na waandishi wa habari hii leo ambapo pia anatarajiwa kulizungumzia suala hilo.
Mwandishi: Isaac Gamba/ RTRE
Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman