Obama ahimiza mshikamano
15 Desemba 2012Obama amesema kwamba mauwaji hayo yaliyofanyika katika jimbo la Connecticut yamesababisha "nyoyo za Wamarekani kuemewa na huzuni " kutokana na maisha yaliyopotea. Katika hotuba yake ya kila wiki kupitia radio na mtandao, Obama pia amerudia ujumbe alioutowa hapo Ijumaa masaa machache baada ya kutokea kwa mauaji hayo ya watu wengi kwa mashambulizi ya risasi, mabaya kabisa kuwahi kushuhudiwa katika historia ya Marekani.Amesema kuna haja ya kuweka kando siasa ili kuchukuwa kile alichosema "hatua madhubuti za kukomesha maafa zaidi kama hayo." Lakini Obama hakwenda mbali zaidi kutowa wito wa kutaka kuwepo kwa sheria kali zaidi za kudhibiti silaha.
Watoto hao 20 wameuliwa na mwanaume mmoja aliekuwa na silaha nzito ambaye aliwafyetulia risasi wakati wakiwa darasani katika shule ya msingi ya mji wa Newtown ulioko katika jimbo la Connecticut hapo Ijumaa. Kwa jumla ameuwa watu 26 akiwemo mwalimu mkuu wa shule hiyo na mwanasaikolojia wa shule kabla ya kujiuwa mwenyewe. Obama amekaririwa akisema " Mwishoni mwa juma hili, Michelle na mimi tunafanya kile ambacho najuwa kitakuwa kinafanywa na kila mzazi -kuwakumbatia watoto wetu kwa kadri inavyowezekana na kuwakumbusha jinsi tunavyowapenda."Obama ameendelea kusema kwamba kuna familia katika jimbo la Connecticut ambazo haziwezi kufanya hivyo leo hii na kwamba familia hizo hivi sasa zinawahitaji. Ameongeza kusema " Sote tunaweza kuwanyoshea mkono wale wenye dhiki kuwakumbusha kwamba tuko kwa ajili yao na kwamba tunawaombea."
Muuaji ni nani ?
Muuaji alietambuliwa na polisi kwa jina la Adam Laza mwenye umri wa miaka 20 alimuuwa mama yake kwanza Nancy Lanza kwa kumpiga risasi nyumbani kwao kabla ya kufanya mauaji hayo shuleni. Polisi inasema inawezekana kijana huyo alikuwa na matatizo ya akili. Hadi sasa serikali haikuzungumza hadharani juu ya kile kinachowezekana kuwa dhamira ya mauaji hayo. Haikugunduwa taarifa yoyote ile iliowachwa na muuaji huyo ambaye alikuwa hana rekodi ya uhalifu.Mashahidi wanasema hakutamka neno lolote lile wakati akifanya mauaji hayo.Wapelelezi wanaamini Lanza aliwahi kusoma katika shule hiyo miaka michache iliopita lakini hakuwa na mawasiliano nayo katika siku za hivi karibuni. Wale waliokuwa wakimfahamu wanamuelezea kuwa alikuwa kijana hodari lakini alikuwa hana maingiliano na wenzake.
Obama atakiwa kuchukuwa hatua
Mauaji hayo yameamsha upya mjadala juu ya udhibiti wa silaha katika nchi ambapo utamaduni wa kumiliki silaha umeshamiri na kuna ushawishi mkuwa wa kupigia debe umilikaji wa silaha, jambo ambalo limewakatisha tamaa wanasiasa wengi kufanya jitihada zozote zile kubwa za kushughulikia tatizo la kumiliki silaha kwa urahisi.
Meya wa mji wa New York Michael Bloomberg ambaye anaongoza muungano wa mameya katika suala la sera ya silaha amesema hapo Ijumaa kwamba Rais Obama wa chama cha Demokrat anapaswa kuchukuwa hatua licha ya upinzani kutoka chama cha Republikan ambacho kinalidhibiti Baraza la Wawakilishi la bunge la Marekani. Bloomberg amesema katika taarifa " Tumeyasikia madoido ya kusema kabla.Hatukushuhudia uongozi sio kutoka Ikulu wala kutoka bungeni. Jambo hilo halina budi kukomeshwa leo hii."
Maafisa wa polisi waliwakuta watoto 18 wenye umri kati ya miaka 6-7 na watu wazima saba akiwemo muuaji wakiwa tayari wamekufa huko shuleni na watoto wawili walifia hospitali kutokana na kujeruhiwa vibaya. Obama amesema wengi waliokufa walikuwa ni watoto wadogo ambao walikuwa na maisha marefu yakiwasubiri na kwamba kila mzazi nchini Marekani moyo wake umeemewa na huzuni. Obama ilibidi ajitahidi kudhibiti hisia zake na kufuta machozi yaliokuwa yakimtoka wakati alipoliambia taifa kupitia televisheni akiwa Ikulu hapo Ijumaa kwamba " Nyoyo zetu zimevunjika." Zaidi ya watu 1,000 hapo Ijumaa wamekesha kucha katika Kanisa la Kikatoliki la St. Rose lilioko maili chache kutoka eneo la mauaji kufanya ibada ya maombi.
Idadi ya vifo hivyo imepindukia ile ya mauaji mabaya kabisa kuwahi kushuhudiwa katika shule za Marekani ya hapo mwaka 1999 ambapo vijana wawili waliwauwa kwa kuwapiga risasi wanafunzi na wafanyakazi 13 katika Shule ya Sekondari ya Littleton katika jimbo la Colorado kabla ya kujiuwa wenyewe. Kwa kiasi kikubwa Obama alikuwa hakuligusa suala la udhibiti wa silaha wakati wa kampeni yake ya kuchaguliwa tena kuwa rais wa Marekani na haijulikani iwapo atakuwa tayari kulishughulikia kwa dhati zaidi hivi sasa baada ya kushinda kipindi cha pili cha urais.
Mwandishi: Mohamed Dahman/RTRE/dpa
Mhariri: Alakonya,Bruce