Obama ahimiza ustahamilivu kesi ya Zimmerman
15 Julai 2013George Zimmerman, mwanaume aliyempiga risasi na kumuuwa kijana mweusi, Trayvon Martin mwenye umri wa miaka 17, aliachiwa huru Jumamosi iliyopita baada ya jopo la mawakili sita wote wa kike kuamua kuwa hakuwa na hatia, lakini bado anakabiliwa na ghadhabu ya umma, na uwezekano wa kufunguliwa mashtaka mapya.
Wanaharakati wa haki za kiraia wamepeleka malalamiko yao katika mahakama ya serikali kuu, na wizara ya sheria imesema inaangalia iwapo inao ushahidi wa kutosha kuunga mkono mashtaka mapya dhidi ya Zimmerman, baada ya kuachiwa huru na mahakama ya jimboni mwake Florida.
Maandamano katika miji kadhaa
Kuachiwa kwake kumezusha maandamano makubwa katika miji kadhaa ya Marekani, ikiwemo New York. Waandamanaji wamebeba mabango yasemao, bila haki, hakuna amani. Mwanamke huyu anasema waendesha mashitaka hucharuka tu, wanapowaandama washukiwa weusi.
''Kitu ambacho hakieleweki hapa, ni kwamba waendeshamashitaka wanafanya kazi nzuri sana wanapowafuatilia washukiwa vijana weusi jimboni Florida, lakini kwa sababu ambazo hatuzielewi, wanashindwa kumpata na hatia Zimmerman. Hatuelewi ilivyotokea''.
Kuuwa kwa kujihami
Mawakili wa Zimmerman wanadai kuwa Trayvon Martin alimshambulia mteja wao, ambaye kwa kujihami alimfyatulia risasi na kumuuwa. Wanawashutumu wanaharakati kuingiza suala la rangi ya ngozi kimakosa katika kesi hiyo. Na kuna wanaokubaliana na maoni hayo.
Ingawa naionea huruma familia ya Trayvon Martin, naamini kuwa jopo la mawakili lilichunguza vizuri ushahidi wote, na limefikia uamuzi sahihi wa kutmkuta na hatia Zimmerman.
Wakosoaji wanasema Zimmerman ambaye ni mweupe, alimshuku Martin kuwa jambazi kwa sababu tu ya rangi ya ngozi yake. Alipiga simu polisi na kuwaarifu kuwa amemuona mtu wa kutilia shaka, kisha akatoka ndani ya gari lake na kumfuata huku akiwa na bunduki iliyojaa risasi. Ugomvi uliibuka kati ya watu hao wawili, Zimmerman akapata jeraha puani na kichwani, naye akampiga Martin risasi moja moyoni na kumuuwa.
Obama aingilia kati
Rais Barack Obama ambaye kwa wakati mmoja alisema kama angekuwa na mtoto wa kiume angefanana na Trayvon Martin, ametoa wito wa kuwepo utulivu. ''Sisi ni taifa linaloheshimu sheria, na mahakama imeamua'' alisema Obama, na kuwataka wamarekani wote kuheshimu rai ya wazazi wa Trayvon, ya kutafakari kwa utulivu yaliyotokea.
Zimmerman ambaye hakuonyesha hisia kubwa pale jopo la mawakili lilipotangaza kuwa sasa ni mtu huru, aliondolewa vifaa vya elektroniki vilivyokuwa vikifuatilia hatua zake alipokuwa nje kwa dhamana. Kaka yake alisema kuwa anapanga kubakia mafichoni kwa muda, na kwamba ana nia ya kusomea sheria. Hata hivyo maoni ya wengi ni kuwa ingawa yuko huru sasa, anakabiliwa na hofu ya watu ambao wanaweza kuamua kuchukua sheria mikononi mwao na kulipiza kisasi.
Mwandishi: Daniel Gakuba/RTRE/AFPE
Mhariri: Ssessanga, Iddi Ismail