1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama aidhinisha makato ya bajeti

2 Machi 2013

Rais Barack Obama wa Marekani ameidhinisha makato ya dola bilioni 85 katika bajeti ya serikali, ambayo yanaweza kuathiri uchumi wa nchi hiyo na kusababisha upotevu wa nafasi za ajira.

Rais Barack Obama baada ya kuidhinisha makato ya bajeti ambayo amesema hayakuwa ya lazima
Rais Barack Obama baada ya kuidhinisha makato ya bajeti ambayo amesema hayakuwa ya lazimaPicha: Reuters

Obama ameichukua hatua hiyo shingo upande, kutekeleza wajibu wake kisheria, ambao utaanzisha mara moja punguo katika bajeti ya kijeshi na matumizi ya ndani, baada ya kushindwa kupata makubaliano na chama cha Republican kuhusu namna ya kumaliza nakisi katika bajeti.

Rais Obama amesema kutimiza makato hayo hakuna budi kufuata kikamilifu sheria ya Marekani na maagizo ya ofisi yake kuhusu punguzo katika kila idara.

Warepublican wanyoshewa kidole

Awali, Rais Barack Obama alikitupia lawama chama cha Republican juu ya kile kilichoitwa bomu la makato ya bajeti linalosubiri kuripuka, akisema chama hicho kiligoma kuziba pengo katika ushuru unaotozwa matajiri na makampuni ya kibiashara, ambao ungeambatana na makato maalum kupata uzani katika kupunguza nakisi.

''Mimi sio Dikteta, mimi ni rais'', alisema Obama, na kuongeza kuwa hawezi kuwashurutisha warepublican kufanya ''yaliyo sahihi'', au kuamuru maafisa wa usalama kuwazuia viongozi wa chama chao ndani ya chumba hadi pale mapatano yatakapofikiwa.

Obama alisema makato hayo yataugharimu uchumi wa Marekani na kupoteza nafasi za kazi, na kuongeza kuwa kila upande unapaswa kulegeza misimamo yake ili marekebisho yaweze kufanywa. Rais huyo amesema kuwa makato hayo hayakuwa ya lazima.

Makato yasio ya lazima

Baraza la Congress litalazimika kupata muafaka kuepusha kusimama kwa shughuli za serikali.Picha: picture-alliance/dpa

Barack Obama alikuwa anawajibika kisheria kuidhinisha makato hayo hadi mwisho wa jana Ijumaa. Makato hayo ambayo yanajulikana kama ''sequester'' yanayolenga hasa sekta ya ulinzi na matumizi ya ndani hayakutazamiwa kutekelezwa, bali yalifikiriwa kama hatua ya kuwalazimisha wabunge wa kambi zinazokinzana kupata muafaka juu ya bajeti ambao ungeyaepusha.

Vyama vyote vinakubaliana kwamba makato hayo ni ''silaha butu'' katika mchakato wa kupunguza makato, ambayo haijui tofauti kati ya mipango ya lazima na ile ambayo ni ya ufujaji. Waziri mpya wa ulinzi wa Marekani Chuck Hagel ameonya kwamba punguo katika bajeti ya ulinzi laweza kulitatiza jeshi la nchi hiyo katika kutekeleza majukumu yake.

Hatua inayofuata ni muswada juu ya fedha za matumizi ya serikali, ambao unapaswa kupitishwa na baraza la Congress ifikapo Machi 27, na bila ya hivyo, shughuli za serikali zitasimama.

Vyama vyote vimeashiria utashi wa kuepusha hali hiyo, na kwa maana hiyo makato ya ''sequester'' yataendela, isipokuwa kama itapatikana njia mbadala ya kupunguza matumizi.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFP/RTRE

Mhariri: Iddi Ssessanga

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW