1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama aikosoa hotuba ya Netanyahu

4 Machi 2015

Rais Barack Obama amemkosoa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kuhusiana na hotuba yake katika bunge la Marekani, kuhusu makubaliano yanayotarajiwa kufikiwa kati ya Marekani na Iran ya mpango wa nyuklia

USA Washington Rede Benjamin Netanjahu Kongress
Picha: Getty Images/AFP/N. Kamm

Obama anasema kuwa muafaka huo unaotarajiwa kusainiwa mwishoni mwa mwezi huu ndio chaguo bora zaidi.

Baada ya Netanyahu kutoa hotuba hiyo katika bunge la Marekani hapo jana, Obama alijibu kwa kusema kuwa kiongozi huyo wa Israel hana mpango wowote mbadala unaoweza kukikabili kitisho hicho cha Iran. Na, wakati Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani John Kerry akifany amazungumzo na mwenzake wa Iran nchini Uswisi, mataifa yenye nguvu duniani yanashinikiza kupatikana muafaka ambao utapunguza uwezo wa Iran wa nishati ya nyuklia, kwa kuondolewa vikwazo vya kiuchumi.

Obama anasema hotuba ya Netanyahu haina chochote kipya, kuhusiana na mpango wa nyuklia wa IranPicha: Getty Images/Guerrucci/Pool

Katika hotuba yake, Netanyahu hakuficha msimamo wake huku akiyapinga makubaliano anayotarajia kuwa Iran itasaini na Marekani kabla ya mwisho wa mwezi huu.

Obama hakutazama hotuba hiyo, kwa sababu alikuwa kwenye kikao alichoandaa kwa njia ya video na viongozi wa Ulaya kuhusu mzozo wa Ukraine, lakini baadaye alitoa hisia zake kuhusu hotuba hiyo.

Wakati wabunge kadhaa wa chama cha Obama cha Democratic wakisusia hotuba hiyo ya Congress, wabunge wengine wengi kutoka pande zote mbili walihudhuria na kumpigia makofi Netanyahu.

Lakini licha ya hayo, baadhi ya Wademocrats walimkosoa kwa kile walichokiita kuwa ni “kuzusha hofu”. Kiongozi wa wabunge wa upinzani wa chama cha Democratic katika baraza la wawakilishi Nancy Pelosi alisema “amehuzunishwa na kile alitaja kuwa ni matusi kwa busara ya taifa la Marekani”.

Wiki mbili kabla ya uchaguzi nchini Israel ambako anawania kuchaguliwa tena, Netanyahu amesema kwamba makubaliano yoyote na Iran yanatishia uhai wa taifa lake. Pia amesema kwamba kiongozi wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, ameandika katika ukurasa wa Twitter kwamba Israel ni lazima iangamizwe. Iran imezipinga kauli za Netanyahu, huku msemaji wa wizara ya mambo ya nje Marzieh Afkhan akimshtumu Netanyahu kwa kueneza uwongo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, ambao serikali ya Iran inasisitiza ni wa amani.

Mwandishi: Bruce Amani/AP
Mhariri: Mohammed Khelef

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW