1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama aionya Libya kujiandaa na hatua za kijeshi

19 Machi 2011

Rais Barack Obama ameonya juu ya matumizi ya nguvu za kijeshi, iwapo kiongozi wa Libya Kanali Muhammar Gaddafi hatosimamisha mashambulizi yake dhidi ya waasi.

Rais Barack ObamaPicha: AP

Rais Obama amesema hakuna mjadala juu ya yale yaliyomo katika azimio lililopitishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambayo ni kuwalinda raia.Ufaransa na Uingereza pamoja na nchi nyengine za kiarabu zinatarajiwa kuongoza juhudi za mashambulizi ya anga dhidi ya Libya

Wakati huo huo viongozi wa mataifa kadhaa duniani wanakutana hii leo huko mjini Paris Ufaransa, kabla ya kufanyika kwa mkutano utakaoamua jinsi ya kutekeleza azimio hilo la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la vikwazo vya anga dhidi ya Libya.

Mkutano huo unawajumuisha viongozi kutoka Umoja wa Ulaya,Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa ya Kiarabu.Viongozi wa mataifa duniani wamesema kuwa ni muhimu kuwalinda wananchi wa kawaida nchini Libya ambao wamenaswa katika mapigano kati ya majeshi yanayomtii kiongozi wa Libya Kanali Mohamar Gaddafi na waasi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton anaudhuria mkutano huo pamoja na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ijapokuwa nchi yake ilisusia kupiga kura juu ya azimio hilo huko New York.

Kansela Merkel alisema hatua hiyo ya Ujerumani kujiondoa katika kupiga kura kusichanganywe na kutoegemea kwa nchi hiyo upande wowote.

Serikali ya Kanali Gaddafi hapo jana ilitangaza kusitisha mapigano, lakini hata hivyo kumekuwa na taarifa za kuendelea kwa mashambulizi dhidi ya mji wa Benghazi ambao ndiyo ngome ya waasi.

Aidha Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Libya Khaled Kaaim amesema waasi hao wamefanya uhalifu dhidi ya binaadamu katika mji huo wa Benghazi.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/DPA

Mhariri:Mohamed Dahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW