Obama aionya Sudan Kusini
22 Desemba 2013Ikulu ya White House ilisema katika taarifa iliyotolewa siku ya Jumamosi kwamba juhudi zozote za kunyakua madaraka kwa kutumia mtutu wa bunduki zitapelekea kukatwa kwa msaada wa muda mrefu kutoka Marekani na jumuiya ya kimataifa.
Obama alisisitiza kuwa viongozi wa Sudan Kusini walikuwa na wajibu wa kuunga mkono juhudi za kuhakikisha usalama wa wanajeshi na raia wa Marekani walioko mjini Juba na Bor - mji mkuu wa jimbo la Jonglei ambao sasa uko mikononi mwa waasi.
Matamshi hayo ya rais Obama yalikuja baada ya helikopta tatu aina ya CV-22 Osprey kushambuliwa wakati zikielekea mjini Bor kusaidia kuwaondoa Wamarekani kutoka Sudini Kusini, ambayo inakabiliwa na kitisho cha vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Shambulio hilo lilisababisha uharibifu kwa ndege hizo, ambazo zililaazimika kubadilisha njia na kuelekea Uganda. Askari waliojeruhiwa walikimbizwa mjini Nairobi kwa ajili ya matibabu, na taarifa ya wizara ya ulinzi ya Marekani ilisema wanaendelea vizuri.
Shambulio hilo lilibainisha hali inayozidi kuwa ya hatari nchini Sudan Kusini, ambako kituo kimoja cha Umoja wa Mataifa kilishambuliwa katika siku za hivi karibuni, na kusababisha vifo vya askari wawili wa kulinda amani kutoka India na raia kadhaa. Marekani, Uingereza, Kenya na Uganda zimekuwa zikiendesha operesheni za kuondoa raia wake nchini Sudan Kusini.
Ban Ki-Moon apandisha sauti
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ametaka kukomeshwa mara moja kwa ghasia, na kuonya kuwa maelfu wanaendelea kuwa hatarini.
"Nawataka viongozi wote wa kisiasa, kijeshi na wa wanamgambo kukomesha vurugu dhidi ya raia," Ban aliuambia mkutano wa waandishi wa habari mjini Manila, Ufilipino, wakati akihitimisha ziara ya siku mbili nchini humo siku ya Jumapili.
Aliwatolea wito rais Kiir na mpinzani wake aliemfukuza Machar, kutafuta suluhu ya kisiasa kuondokana na mgogoro huu, na kuwaamrisha wafuasi wao kuweka chini silaha. Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alisema kuendelea kwa vurugu, ziwe za kikabila au vinginevyo hakukubaliki kabisaa, na kunatishia mustakabali wa taifa lao changa.
Uchimbaji mafuta hatarini
Kampuni za mafuta pia zimeondoa wafanyakazi wake, baada ya kuuawa kwa wafanyakazi wasiopungua wanne, raia wa Sudan Kusini siku ya Jumatano. Uchimbaji wa mafuta unachangia asilimia 95 katika uchumi wa taifa hilo, na sasa wataalamu wanaonya kuwa waasi wanatishia visima muhimu, jambo ambalo linaweka uwezekano wa kuingilia kijeshi kutoka kwa Sudan, iwapo visima hivyo havitalindwa.
Siku ya Jumamosi, kamanda muhimu katika udhibiti wa jimbo la Unity, ambalo ni mmoja ya maeneo muhimu zaidi ya uchimabji wa mafuta, aliasi na kujiunga na vikosi vitiifu kwa Riek Machar. Msemaji wa jeshi Philip Aguer alisisitiza kuwa vikosi vitiifu kwa rais Salva Kiir bado vinalidhibiti jimbo la Unity - ikiwa ni pamoja na visima vyake vya mafuta - na kwamba ni mji mkuu tu wa jimbo Bentiu ndiyo uliyoangukia mikononi mwa waasi.
Lakini wakati wafanyakazi wakikimbia, kuupoteza mji mkuu wa jimbo katika eneo lililojaa silaha na lenye historia ndefu ya uasi ni pigo kubwa. "Uwezekano wa utajiri wa mafuta kuchochea mapambano ya sasa ya madaraka haupaswi kudharauliwa," alisema Emma Vickers kutoka shirika la Global Witness na kufafanua kuwa "kama vikosi vya waasi vitadhibiti visima vya mafuta, basi vitaishikilia mateka serikali."
Sudan yahofia kusitishwa kwa usafirishaji
Tayari Sudan imesema inahofia hatma ya nishati muhimu ya mafuta. Uchumi wake unaokabiliwa na matatizo makubwa unatarajia kupokea kiasi cha dola za Marekani bilioni 1.5 katika malipo kutoka Sudan Kusini mwaka ujao kwa kusafirisha mafuta ghafi kupitia mabomba yake kwa ajili ya mauzo ya nje.
"Tukio baya zaidi kwetu ni iwapo vita hivi vitasambaa katika maeneo mengine, hili litakuwa na athari kubwa sana kwetu," alisema waziri wa mawasiliano wa Sudan Ahmed Bilal Osman siku ya Ijumaa na kuongeza kuwa udhibiti wa visima vya mafuta litakuwa lengo muhimu kwa wanaopigana, ili kuweza kuimarisha nafasi yao katika majadiliano.
Wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya mwaka 1983 - 2005, serikali mjini Khartoum iliyaunga mkono makundi ya wanamgambo dhidi ya jeshi la uasi la Kusini, ambalo sasa --baada ya uhuru wa Kusini mwaka 2011, ndilo jeshi rasmi la serikali. Mengi ya makundi hayo ya kulinda visima yaliingizwa katika jeshi la Sudan Kusini, lakini wakati ambapo baadhi ya vikundi vya jeshi vikiasi, huenda baadhi nao wamegeukia uasi.
Baada ya mapigano makali ya mpakani mwaka uliyopita, na madai kwamba Sudan Kusini ilikuwa ikiwaunga mkono waasi nchini Sudan, uhusiano baina ya mataifa hayo mawili uliboreka baada ya mkutano kati ya marais Kiir na Omar al-Bashir. Viongozi hao wawili waliahidi kutekeleza makubaliano kadhaa ya kiusalama na kiuchumi.
Yatahadharishwa kutoingilia kati
Lakini makubaliano hayo "yatakuwa magumu kutekelezeka kama huna mshirika mjini Juba," alisema mwanadiplomasia moja ambaye hakutaka jina lake litajwe. "Sudan inaweza kutumia migogoro ya ndani ya Sudan Kusini kwa manufaa yake, licha ya kuhakikisha huko nyuma kwamba nchi hizo mbili hazitaathiriwa na migogoro ya kisiasa nchini Sudan Kusini," alisema Ahmed Soliman kutoka shirika la ushauri la Uingereza Chatham House.
Wakati Sudan ikishiriki juhudi za upatanishi, wanadiplomasia wa kigeni mjini Khartoum wanasema hakuna kikubwa sana ambacho inaweza kufanya kusitisha ghasia, na jaribio lolote la kuingilia kati lina hatari ya kuvuruga zaidi hali.
"Wanapaswa kuepuka kishawishi chochote - kama kipo- kujihusisha katika mgogoro huo," alisema mwanadiplomasia mwingine wa kigeni mjini Khartoum. "Hilo linaweza kuishia tu katika maafa."
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe
Mhariri: Abdul Mtullya