1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama akabiliwa na wakati mgumu Mashariki ya Kati

13 Mei 2011

Huku Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, akielekea Washington hivi karibuni, Rais Barak Obama anakabiliwa na maamuzi magumu juu ya kutimiza ahadi yake ya suluhu ya mataifa mawili huru ya Israel na Palestina.

Rais Barack Obama
Rais Barack ObamaPicha: AP

Changamoto inayomkabili Rais Obama imeonekana kuwa ngumu zaidi kufuatia matukio ya hivi karibu na hasa maridhiano yaliyofikiwa hivi karibuni kati ya Hamas na Fatah chini ya upatanishi wa Misri.

Maridhiano hayo yameungwa mkono na pande zote za utawala wa Palestina na kundi la Hamas ambalo serikali ya Marekani inaliangalia kama la kigaidi.

Rais Mahmoud Abbas wa Palestina amelitaka pia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuitambua Palestina kama dola wakati litakapoanza vikao vyake mwezi Septemba.

Rais Mahmoud Abbas wa PalestinaPicha: picture alliance/dpa

Hatua zote hizo zimepingwa na kulaaniwa na serikali ya Netanyahu na kulaaniwa kwa nguvu zote na wale wanaojulikana kama ni "wapiga-debe wa Israel", ambao wanaungwa mkono na wabunge wa kutosha ndani ya mabunge yote mawili ya Marekani.

Tayari wabunge wa ngazi ya juu katika mabunge hayo wameshatishia kuondoa msaada wa kiasi cha dola milioni 400 unaotolewa kila mwaka kwa Mamlaka ya Palestina, hadi pale utawala huo utakapotafakari kubatilisha uamuzi wake wa kushirikiana na Hamas.

Aidha wabunge hao wamemtaka Rais Obama kupinga juhudi za Palestina za kutaka kuwa na dola huru. Lakini wataalamu wa masuala ya Mashariki ya kati wanahisi hiyo ni hatua ambayo Marekani haitakiwi kabisa kuichukua.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin NetanyahuPicha: AP

Mara kadhaa Rais Abbas ana matumaini makubwa kwamba Uingereza na Ufaransa zitaunga mkono hatua ya Palestina kuwa dola huru mnamo Septemba katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Anasema kwamba Palestina itatumia nafasi hiyo kumtaka Rais Obama kutimiza ahadi zake.

Wataalamu wanasema wakati ambapo Marekani inazitaka nchi za Kiarabu kuwajibika katika kutekeleza matakwa ya watu wao, kupinga mshikamano wa Wapalestina ambayo ni hatua iliyokuwa ikililiwa na Wapalestina kwa miaka mingi sasa, kutatuma ujumbe mbaya kwa Wapalestina na kwa ulimwengu wa Kiarabu kwa jumla.

Aliyekuwa mpatanishi katika masuala ya kutafuta amani, Aaron David Miller, anasema Rais Obama anahitajika kuchukua hatamu za kudhibiti diplomasia ya Mashariki ya Kati.

Netanyahu atalihutubia bunge la Marekani mnamo Mei 24 kama alivyodokeza spika wa bunge hilo, John Boehner. Boehner ameongeza kusema kwamba Marekani na Israel ni marafiki na washirika wa dhati na kwamba hotuba ya Netanyahu inasubiriwa kwa hamu na bunge lake.

Kabla ya hapo, Netanyahu atakuwa na mazungumzo na Rais Obama katika Ikulu ya Marekani tarehe 20 Mei.

Mwandishi: Saumu Mwasimba /IPS
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW