Obama amlaumu Assad kupoteza fursa ya mageuzi
13 Julai 2011Akizungumza na kituo cha televisheni cha CBS, Rais Obama pia ameyalaani mashambulizi dhidi ya ubalozi wa Marekani mjini Damascus. Rais Obama amesema nchi yake imeipelekea serikali ya Syria ujumbe wa wazi kwamba "haiwezi kuvumilia uvamizi wa balozi zake" na kwamba ni jukumu la serikali hiyo kutoa ulinzi wa uhakika kwa balozi za kigeni nchini mwake.
Wakati huo huo, msemaji wa wizara ya nje ya Marekani, Victoria Nuland, amesema balozi wa Marekani mjini Damascus, Robert Ford, amekutana na naibu waziri wa mambo ya nje wa Syria kwa mazungumzo yaliyotajwa kuwa ya "ushirikiano."
Hapo jana (12 Julai 2011), Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, lililaani vikali kushambuliwa kwa balozi za Marekani na Ufaransa nchini Syria kulikofanywa na watu wanaoshukiwa kuwa wafuasi wa Rais Assad hapo Jumatatu.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP
Mhariri: Sekione Kitojo