1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama aongoza kumbukumbu ya "D-Day"

Mohamed Dahman7 Juni 2014

Rais Barack Obama wa Marekani ameongoza kwa unyenyekevu kumbukumbu ya kutowa heshima zao kwa maelfu ya wanajeshi waliojitolea maisha yao kuikomboa Ulaya kutoka kwa Manazi ikiwa ni miaka sabini ya siku ya D-Day.

Rais Barack Obama wa Marekani katika kumbukumbu za miaka 70 ya D-Day huko Normandy Ufaransa. (06.06.2014)
Rais Barack Obama wa Marekani katika kumbukumbu za miaka 70 ya D-Day huko Normandy Ufaransa. (06.06.2014)Picha: Damien Meyer/AFP/Getty Images

Akizungumza katika pwani ya Omaha Ijumaa (06.06.2014)mbele ya maveterani waliovalia sare za kieshi zikiwa na medali zinazon'gara kutokana na mwanga wa jua,Obama amesema kujitolea kwao muhanga na ushujaa wao umeuvunja "Ukuta wa Hitler " na kuweza kufanikisha kwa enzi ya demokrasia na uhuru iliopo hivi sasa.

Obama aliyeonekana kuguswa na kile alichokuwa akikizungumza na kushangiliwa mara kwa mara amesema kufikia mwisho wa siku hiyo refu , fukwe hiyo ilipiganiwa, ikapotezwa na kupiganiwa tena na kushinda, sehemu ya Ulaya ikakombolewa kwa mara nyengine tena na kuwa huru.Ukuta wa Hitler ukavunjwa na kuliwezesha jeshi la Patton kumiminika Ufaransa.

Rais huyo wa Marekani ameongeza kusema kwamba pwani hiyo ya Omaha ilioko Normandy ni pwani ya demokrasia na kwamba ushindi wao katika vita hivyo sio tu umepatikana karne moja tu iliopita ,bali umejenga taswira mpya ya usalama na ustawi wa binaadamu.

Maveterani watukuzwa

Baada ya hotuba yake hiyo Obama alimkumbatia veterani mmoja aliepigana katika mapambano hao ya D-Day miaka sabini iliopita kabla ya kuinamisha kichwa chake pamoja na Rais Francois Hollande wa Ufaransa katika uwekaji wa mashada ya mauwa kwa kumbukumbu ya maelfu ya waliouwawa katika vita vya Juni sita mwaka 1944.

Rais Barack Obama wa Marekani na Rais Francois Hollande wa Ufaransa katika kumbukumbu za miaka 70 ya D-Day huko Normandy Ufaransa. (06.06.2014)Picha: Damien Meyer/AFP/Getty Images

Viongozi hao wawili baadae walisimama mikono ikiwa wameshikilia nyoyo zao kuwapigia saluti maveterani waliokuwa wamesimama nyuma yao huku tarumbeta likipigwa na ndege za kivita zikivinjari angani.

Kwa upande wake Rais Francois Hollande wa Ufaransa amesema Ufaransa katu haitosahao deni la fadhila la Marekani.Amesema "Ufaransa katu haitosahau deni ililonalo kwa wanajeshi hao,deni ililonalo kwa Marekani. Ufaransa haitosahao kamwe mshikamano kati ya mataiha haya mawili."

Malkia wa Uingereza aongoza maombi

Malkia Elizabeth wa Pili wa Uingereza aliongoza maombi katika makaburi ya Bayeux ambapo wanajeshi wa nchi za Jumuiya ya Madola 5,000 walizikwa.

Waziri Mkuu wa Ufaransa Manuel Valls(kushoto), Malkia Elizabeth wa Pili wa Uingereza (katikati) na Mwana mrithi wa Ufalme wa Uingereza Charles (kulia) katika kumbukumbu ya miaka 70 ya D-Day huko Normandy,Ufaransa. (06.06.2014).Picha: Reuters

Malkia huyo wa Uingereza aliyevalia koti la kijani ya ndimu na kofia inayolingana na rangi hiyo anafanya ziara hiyo ya kigeni ya nadra akiwa na umri wa miaka 88.

Takriban viongozi 20,wafalme na mawaziri wakuu walichanganyika na maveterani katika sherehe za kumbukumbu hiyo kaskazini mwa Ufaransa ambapo shambulio kubwa kuwahi kushuhudiwa katika historia la baharini na nchi kavu lilifanyika hapo mwaka 1944.

Mwandishi: Mohamed Dahman /AFP

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman