1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama apiga kura ya mapema

26 Oktoba 2012

Rais Barack Obama wa Marekani amepiga kura yake kwa ajili ya uchaguzi wa Novemba 6, katika mji wake wa nyumbani wa Chicago, na kutoa wito kwa wengine wanaoweza kufanya hivyo kabla ya siku ya uchaguzi kuiga mfano wake.

Uchaguzi umeanza katika baadhi ya majimbo nchini Marekani.
Uchaguzi umeanza katika baadhi ya majimbo nchini Marekani.Picha: picture-alliance/dpa

Hatua hiyo ya jana inamfanya Obama kuweka historia nyingine ya kuwa rais wa kwanza nchini Marekani kupiga kura ya mapema. Obama alipiga kura yake wakati wa ziara fupi katika mji wa Chicago wakati akiwa katika kampeni ya majimbo manane. Baadaye alihutubia mkutano wa usiku katika jimbo la Ohio, moja ya majimbo yenye maamuzi katika mchuano huu mkali kati yake ya mgombea wa chama cha Republican, Mitt Romney, ambapo kura za maoni zinaonyesha wagombea hao wawili wanakabana koo.

Mitt Romney na rais Obama katika mjadala wa wazi.Picha: Reuters

Mchambuzi kutoka Chuo Kikuu cha George Mason, Michael McDonald anaeleza umuhimu wa kura hii ya mapema: "Kampeni zinajua nani amepiga kura na hii inawapa fursa ya kuondoa majina yao katika orodha ya watu wanaotaka kuwasiliana nao na kuweza kuangalia watu katika orodha hizo ambao ni wagumu wa kupiga kura ili waweze kuwaendea na kuwashawishi wapige kura."

Majimbo 34 yaanza kupiga kura

Obama alisema nchini Marekani kote watu walikuwa wanapiga kura ya mapema na kuongeza kuwa hii inawaweka huru wapiga kura kutokana na kufikiri namna ya kuwatunza watoto wao wakati wa kupiga kura, na wengine kuwaza kuchukua siku za mapumziko kazini kwa ajili hiyo Jumanne ya Novemba 6. Akiwa katika ofisi moja ya kampeni, Obama aliwaonya wafuasi wake kuwa wakijisahau na wapiga kura wao wasijitokeze kwa wingi, wanaweza kushindwa uchaguzi na kuongeza kuwa kama wapiga kura watajitokeza kwa wingi kupiga kura ya mapema, bila shaka watashinda.

Katika majimbo 34 pamoja na wilaya ya Shirikisho ya Columbia siku ya Alhamis ilikuwa ni siku ya uchaguzi na raia wataendelea kupiga kura hadi Novemba 6, kwa sababu majimbo hayo yanaruhusu uchaguzi wa mapema. Katika jimbo muhimu la Colorado, karibu asilimia 80 ya wapiga kura watapiga kura yao mapema, kwa hivyo kama wagombea wanataka kuwashawishi wapiga kura hao wanapaswa kufanya hivyo wakati huu.

Raia wa Marekani wakipanga foreni kusubiri kupiga kura.Picha: Getty Images

Kura ya mapema yamnufaisha Obama

Kambi ya Obama inasema takwimu zinaonyesha yeye ananufaika zaidi na kura za mapema. Msemaji wa kampeni yake Jen Psaki alisema matokeo ya kura hii ya mapema yanaonyesha Obama alikuwa anafanya vizuri kuliko ilivyokuwa mwaka 2008 na kwamba alikuwa akimshinda Romney. Alisema rais alikuwa anaongoza katika kura za mapema katika majimbo ya Iowa, Ohio na Wisconsin, na kwamba alikuwa mbele kwa asilimia kati ya 15 hadi 35 miongoni mwa wale waliokwisha piga kura zao.

Lakini Romney naye ameongeza jitihada za kuwashawishi wafuasi wake kuwa ni yeye na wala siyo rais Obama anayestahili kukaa katika ikulu ya White House kwa miaka minne ijayo. Romney anasema Marekani inakabiliwa na uchumi mbaya kwa sababu ya sera mbaya za Obama, wakati Obama anaonya kuwa Wamarekani wametoka mbali na uchumi uliodorora kwa hivyo hawawezi kufanya makosa ya kumuamini Mitt Romney.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe, rtre,dpae
Mhariri: Joseph Nyiro Charo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW