1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama asema Assad hana budi bali kuondoka madarakani

30 Septemba 2015

Rais wa Marekani Barack Obama amesema kiongozi wa Syria Bashar Al Assad hana budi kuondoka madarakani ili vita dhidi ya wanamgambo wenye itikadi kali wa kundi la dola la kiislamu IS viweze kufanikiwa.

Picha: AFP/Getty Images/J. Samad

Maafisa wa Ufaransa kwa upande wao wameanzisha uchunguzi dhidi ya utawala wa kiongozi huyo wa Syria kwa madai ya kuhusika katika uhalifu wa kivita kati ya mwaka 2011 na 2013.

Siku moja baada ya kutofautiana na Rais wa Urusi Vladimir Putin kuhusu hatma ya Assad, Obama aliongoza mkutano hapo jana pembezoni mwa mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa kujadili namna ya kukabiliana na ugaidi, mwaka mmoja tangu kuanzisha kampeini ya mashambulizi ya kijeshi ya angani nchini Syria na Iraq kupambana na IS.

Obama asema kiongozi mpya anahitajika Syria

Obama amesema kuwashinda wanamgambo hao wa IS kunahitaji kuwepo kiongozi mpya Syria na kuwahimiza viongozi wengine wa dunia kumuunga mkono kukabiliana na wanamgambo hao wa IS.

Rais wa Marekani Barack Obama na wa Urusi Vladimir Putin wana msimamo tofauti kumhusu AssadPicha: Reuters/M. Segar

Urusi ambayo ni mshirika mkubwa wa Rais Assad na ambayo imeahidi kumsaidia kijeshi kupambana dhidi ya wanamgambo wa IS, iliususia mkutano huo uliohudhuriwa na takriban viongozi 100 na badala yake inatarajiwa kuendesha mkutano maalum hii leo wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kujadili kitisho cha ugaidi na jinsi ya kukabiliana nao.

Hatma ya Assad katika mustakabali wa siku za usoni wa Syria ndiyo chanzo cha mvutano kati ya Marekani na washirika wa Syria Urusi na Iran huku kukiwa na juhudi kabambe za kidiplomasia kujaribu kuvitatua vita vya Syria ambavyo vimedumu kwa miaka minne na kusababisha vifo vya zaidi ya watu laki mbili na elfu arobaini.

Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Laurent Fabius amesema wameanzisha uchunguzi kutokana na ushahidi uliotolewa na mpiga picha wa zamani wa jeshi la Syria aliyepewa jina Ceaser ambaye aliasi jeshi na kutoroka mwaka 2013 akiwa na zaidi ya picha 55,000 zinazoonyesha vitendo vya kikatili na kinyama vya vita hivyo vya Syria vinavyodaiwa kufanywa na utawala wa Assad.

Naye waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia Adel al Jubeir amesema Assad sharti aondoke madarakani la sivyo ataondolewa kwa nguvu za kijeshi. al Jubeir ameonya kuwa nchi nyingine zitaimarisha misaada kwa waasi wa Syria wenye misimamo ya wastani na hivyo kumlazimu Assad kukosa namna nyingine bali kuachia ngazi.

Huku hayo yakijiri, nchi saba zenye nguvu zaidi za kiuchumi duniani G7 zikiongozwa na Ujerumani pamoja na nchi za Ghuba, zimeahidi kutoa misaada ya kifedha ya kima cha dola bilioni 1.8 kwa mashirika ya kutoa misaada na kushughulikia wakimbizi ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya wakimbizi.

Japan haiko tayari kuwapokea wakimbizi

Wakati huo huo, Japan pia imetangaza msaada wa dola bilioni 1.5 kuwasidia wakimbizi wa kutoka mashariki ya kati lakini waziri mkuu wake Shinzo Abe amesema nchi yake haiko tayari kuwapokea wakimbizi hivi sasa.

Waziri mkuu wa Japan Shinzo AbePicha: Reuters/I. Kato

Zaidi wa wasyria milioni nne wametorokea nchi jirani na maelfu ya wengine wameingia barani Ulaya kutafuta maisha mapya. Kamishna mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu wakimbizi Antonio Guterres ameishukuru Ujerumani na nchi nyingine wafadhili kwa kuongeza misaada yao ya kifedha kuwasaidia wakimbizi.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon atafanya mkutano hii leo kuhusu wakimbizi na wahamiaji pembezoni mwa mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Waziri mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu ambaye nchi yake inawahifadhi wakimbizi milioni mbili kutoka Syria anatarajiwa kuhutubia katika mkutano huo utakaohudhuriwa na viongozi kutoka takriban nchi sabini.

Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters/dpa

Mhariri: Iddi Ssessanga

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW