1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama ataka suluhisho la bajeti haraka

Josephat Nyiro Charo9 Oktoba 2013

Rais Obama amesema yuko tayari kuzungumza na wajumbe wa chama cha Republican kuhusu kitu chochote, lakini baraza la wawakilishi linatakiwa kwanza lipitishe mswaada kuzifungua tena shughuli za serikali.

U.S. President Barack Obama speaks about the continuing government shutdown from the White House Briefing Room in Washington, October 8, 2013. REUTERS/Kevin Lamarque (UNITED STATES - Tags: POLITICS BUSINESS HEADSHOT)
Rais wa Marekani, Barack ObamaPicha: Reuters

Rais wa Marekani, Barack Obama, ameonya kwamba viongozi wa dunia wana wasiwasi wabunge wa chama cha Republican nchini humo huenda wakauvuruga kabisa uchumi wa taifa na kuapa kutotetereka katika msimamo wake wa kutaka kiwango cha fedha Marekani inazoweza kukopa kulipa madeni yake kiongezwe bila masharti yoyote.

Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari katika ikulu yake mjini Washington hapo jana, rais Obama amewataka wabunge wa chama cha Republican waache vitisho na waupigie kura muswaada wa sheria kuidhinisha fedha kwa ajili ya serikali, ambao ikiwezekana huenda ukapitishwa leo.

"Baraza la wawakilishi linatakiwa kupiga kura leo. Kama wanasiasa wa chama cha Republican na spika Boehner wanasema hakuna kura za kutosha. Basi wanatakiwa wathibitishe. Acha muswada upigiwe kura halafu tuone kitakachotokea. Wasiwasi wangu mkubwa ni kwamba kuna kura za kutosha."

Boehner akataa kujisalimisha bila masharti

Spika wa bunge la Marekani, John Boehner, amesisitiza hakutakuwa na 'kujisalimisha bila masharti' kwa chama cha Republican. Boehner amesema bunge litairuhusu Marekani ikope fedha zaidi kama rais Obama atakubali kubana matumizi. Hata hivyo kulikuwa na ishara ya matumaini ya kuutanzua mgogoro mkali wa bajeti ambao umesababisha baadhi ya shughuli za serikali kufungwa kwa zaidi ya wiki moja na hivyo kuibua hofu kwamba Marekani huenda ikashindwa kulipa madeni yake kama kiwango hicho hakitaongezwa kufikia tarehe 17 mwezi huu.

Spika wa bunge la Marekani, John BoehnerPicha: picture-alliance/dpa

Obama amesema kukiwa na haja atakubali makubaliano ya muda mfupi kuongeza kiwango cha fedha serikali inazoweka kukopa na kufungua tena shughuli zilizofungwa, hatua ambayo itauahirisha mkwamo huo kwa wiki kadhaa. Wakati huo huo, rais Obama amewashutumu wabunge wa chama cha Republican kwa kuutumia mkwamo wa bajeti kama chombo cha shinikizo kwa lengo la kuyahujumu mageuzi ya bima ya afya.

Wachambuzi wanasema hiyo ni mbinu mpya ya chama cha Republican kumbana Obama. Mwanauchumi Steven Ricciuto anasema, "Nadhani huo utakuwa mkakati wa chama cha Republican ambao kwa kiwango fulani unaweza kukubalika na Wamarekani; kwamba hupaswi kushindwa kulipa madeni. Lakini katika miswaada yote ya bajeti huenda kuna masharti yaliyofungamanishwa, ambayo huenda yakauendeleaza mkwamo uliopo."

Lakini rais Obama ameshikilia msimamo wake kwamba katu hatokubali makubaliano yoyote kuhusu kukakataa kuzikubali nadharia za chama cha Republican ili apate mamlaka zaidi kukopa fedha kugharamia kifedha majukumu ya Marekani. Obama amesema bunge lina kazi mbili za msingi - kupitisha bajeti na kuhakikisha Marekani inalipa madeni yake. Ameonya kwamba wabunge hawakudai walipwe fidia na kusisitiza msimamo wake kuwa atafanya mazungumzo na Warepublican mara tu kiwango cha fedha kitakapoongezwa na shughuli za serikali zilizofungwa zitakapofunguliwa.

Spika Boehner alijitokeza kwenye televisheni muda mfupi baada ya Obama kumaliza mkutano wake na waandishi wa habari na kusema mazungumzo yatafanyika. Spika huyo pia ameukosoa msimamo wa Obama akisema sivyo serikali ya Marekani inavyofanya kazi. Obama ambaye alizungumza na Boehner hapo kabla kwa njia ya simu, anahoji kuongeza kima cha fedha serikali inazoweza kukopa ni muhimu kwa uaminifu wa taifa hilo kuweza kukopa fedha na hakupaswi kuvurugwa na wasiwasi wa kisiasa.

Mwanamke wa kwanza kuingoza benki kuu ya Marekani

Wakati mzozo wa bajeti ukiendelea, rais Obama leo atamteua Janet Yellen kama mwanamke wa kwanza kuiongoza benki kuu ya Marekani. Obama atampendekeza Yellen kwa awamu ya miaka minne kuchukua mikoba kutoka kwa Ben Bernanke, ambaye sera zake za miaka minane zilihusishwa na kukabiliana na mzozo wa kiuchumi ulioikabili dunia na kutafuta njia za kuufufua uchumi.

Janet YellenPicha: picture-alliance/dpa

Afisa wa Marekani amesema tangazo hilo litafanywa katika ikulu ya Marekani leo usiku katika tukio litakalohudhuriwa na Bernanke, na hivyo kufungua mlango kwa mchakato wa kuthibitishwa katika nafasi hiyo. Yellen, mwenye umri wa miaka 67, amekuwa akishikilia nafasi ya pili ya uongozi wa benki hiyo.

Yellen alizaliwa New York na ameolewa na mshindi wa tuzo ya uchumi ya Nobel, profesa George Akerlof na ni mama wa profesa wa uchumi, Robert Akerlof. Alisomea uchumi katika chuo kikuu cha Brown na baadaye katika chuo kikuu cha Yale, ambako alipata shahada yake ya uzamili. Yellen amekuwa profesa katika chuo kikuu cha Havard na hivi karibuni katika chuo kikuu cha California, Berkeley, ambako mume wake pia hufundisha na kufanya utafiti.

Mwandishi: Josephat Charo

Mhariri: Iddi Ssessanga