Obama atamba mbele ya Clinton
13 Februari 2008Mgombea-wadhifa wa urais wa Marekani kwa chama cha Democratic party- Barack Obama, alishinda jana katika mikoa 3 na sasa amempiku mgombea mwenzake kwa chama hicho seneta Hilary Clinton kwa kudhibiti wajumbe wengi zaidi wa chama chake.
Obama na mtetezi wa wadhifa huo kwa chama tawala cha Republican -John McCain, wametamba katika mikoa ya Virginia,Maryland na District of Columbia.
Kwa ushindi wa Barack Obama ambae baba yake ni wa asili ya kabila la Luo nchini Kenya,ametanua ushindi wake hadi mikoa 8 mfululizo dhidi ya seneta Hilary Clinton,mpinzani wake mkubwa katika kunyan'ganyia nani kati yao atakiwakilisha chama cha Democratic party kuania urais.Isitoshe, amekusanya sasa wajumbe wengi zaidi kumpita Hilary Clinton,mke wa rais wa zamani Bill Clinton.Ni wajumbe hao ambao watamchagua mmoja kati yao hapo August mwaka huu katika kikao maalumu cha chama.
Seneta Obama baada ya ushindi wake wa jana aliwaambia wafuasi wake huko Madison ,Wisconsin ambako changamoto inayokuja itafanyika wiki ijayo:
"Huu ndio wingi mpya wa umma wa Marekani."
"Hivi ndivyo mabadiliko yanayoonekana yakianzia chini kwa wananchi."
Akasema,
"Tunawaletata pamoja wademocrat,wale wasioegemea chama chochote na baadhi ya wanachama wa chama cha Republican."
Akaongeza,
"Nimejua hayo wakati nikipeana mikono kuna mmojawao kule ni shabiki wa Obama alieninon'goneza kuwa "sisi ni waobama wa chama cha Republican".Tunakuungamkono.Asante."
Akijiandaa kushinda katika kura ijayo katika jimbo la Texas,mpinzani wake bibi Hilary Clinton,aliahidi :
"Nataka kuhakikisha kila muamerika anaefanya kazi kikamilifu anajipatia kima cha chini kabisa cha dala 9 na centi 50."
Bibi Clinton aliahidi kwamba watashinda katika kura ya wiki 3 zijazo huko Texas na baadae, watatangaza kile Marekani ionachohitaji-yaani-rais ambae siku yake ya kwsanza tu Ikulu amejiwinda tayari kumudu jukumu lake akiwa kama kamanda mkuu na tayari kuufufua uchumi."Nimeshaonesha uwezo wangu" -alisema Bibi Clinton na "nimejiandaa na nyinyi mshughulikie ninayoahidi yatatekelezwa."
katika kura ya jana watetezi hao 2 wa chama cha Democrat waliania sauti za wajumbe 168 na Obama ameshatia kibindoni sauti za wajumbe 1,074 wakati Bibi Clinton ana jumla ya kura 967 ambazo ni kasoro sana kuweza kuzoa kura 2,025 ambazo lazima kila mtetezi wa urais ajipatie kupewa tikiti ya chama cha Democrat kugombea uchaguzi wa rais hapo Novemba,mwaka huu.
►