Obama atangaza leo mkakati wake kuelekea Afghanistan
3 Desemba 2009Huko Marekani kuna mabishano juu ya mustakbali wa shughuli za kijeshi za nchi hiyo katika Afghanistan. Mkuu wa majeshi ya Marekani kwenyewe huko Afghanistan, Jenerali McChrystal, ametaka watumwe wanajeshi 30,000 zaidi huko Afghanistan ili kuweza kupambana kwa ubora zaidi na ugaidi wa mtandao wa al-Qaida. Leo Rais Obama atautangaza mkakati wake wa siku za mbele kuelekea Vita vya Afghanistan.
Lini majeshi ya Marekani yataondoka Afghanistan? Kwa miezi sasa Wamarekani wanangoja jibu la suali hilo kutoka kwa rais wao. Lakini katika wiki zilizopita, rais huyo hajakubali kubinywa atoe jawabu, mara kadhaa amekutana na majenerali, mabingwa wa usalama na washauri wake. Leo Rais Barack Obama, wakati atakapowahutubia wanafunzi katika chuo cha kijeshi cha Westpoint, atauelezea mkakati wake kuelekea Afghanistan. Hotuba yake itatangazwa kupitia televisheni. Na kutokana na ziara iliofanywa siku chache zilizopita na waziri mkuu wa India, Manmohan Singh, rais huyo, angalau, amedokezea nini yatakuwa malengo yake katika huo mkakati wake wa kuelekea Afghanistan:
" Nataka kukwambieni kwamba maslaha yetu ya kimbinu ni kuhakikisha kwamba al-Qaida na washirika wao wenye siasa kali hawawezi kufanya kazi kwa uzuri."
Wachunguzi wengi mjini Washington wanachukulia kwamba wanajeshi wa Marekani huko Afghanistan wataengezwa kwa idadi ya 30,000 hadi 34,000, kabla ya kupita miaka fulani hivi waweze kuanza kuondoshwa kabisa kutoka nchi hiyo. Pia mabingwa huko Marekani wanasema kwamba Rais Obama ataziomba nchi shirika na Marekani ziongeze wanajeshi wao kwa hadi 10,000. Kinachoingia akilini ni kwamba majeshi ya nchi za NATO huko Afghanistan yatazidishwa kwa askari 5,000 zaidi.
Hata hivyo, hamna mtu aliye na suluhisho rahisi kwa mzozo wa Afghanistan, hata rais mwenyewe.
Bila ya kujali muelekeo gani Rais Obama atakaouchukuwa, lawama zitakuweko. Chama cha upinza ni cha Republican kinatia na kutoa. Kinamtaka Barack Obama afuate pendekezo lilotolewa na mkuu wa majeshi ya Kimarekani katika Afghanistan, Stanley McCrystal. Yeye alitaka wanajeshi ziyada 40,000 kupambana na al-Qaida huko Afghanistan.
Kuna watu wanaohisi kwamba Afghanistan ni nchi muhimu sana katika mapambano dhidi ya ugaidi wa kimataifa, lakini sababu hiyo sio inayoamuwa kila kitu.
Richard Haass wa kutoka Baraza la masuala ya kigeni, aina ya mkusanyiko wa bongo za Wamarekani katika masuala ya siasa za kigeni, anasema kweli Afghanistan ni muhimu, lakini nchi hiyo sio muhimu sana kwa mustakbali wa Marekani au kwa usalama wa Marekani. Afghanistan sio kitu maalumu kwa mtu yeyote, isipokuwa gaidi. Na sio kweli kwamba Afghanistan ina mchango muhimu wa kutoa katika juhudi zinazochkuliwa duniani kupambana na ugaidi. Bwana Haass pamoja na watu wengine wa Chama cha Democratic wanapinga kuengezwa majeshi ya nchi yao huko Afghanistan, wakidai Afghanistan sio nchi pekee ambako magaidi wana kambi zao. Al-Qaida tayari inafanya operesheni zake huko Yemen na Somalia, wanadai wahakiki hao. Bwana Haass anahoji kwamba inamgharimu mlipa kodi wa Kimarekani dola milioni moja kila mwaka kwa kila mwanajeshi mmoja wa Kimarekani anayepigana Afghanistan.
Pia Rais Obama leo atahitaji aelezee vipi atakavoweza kugharimia nyongeza ya majeshi huko Afghanistan.
Na kuna wale wanaohoji kwamba rushwa na uhalali ni vitu vinavokwenda sambamba. Serekali ya Rais Karzai huko Afghanistan imepoteza sana uhalali. Vipi Afghanistan inaweza kufanya kazi katika miaka ijayo bila ya kuweko rushwa nchini humo? Jibu la suali hilo pia Rais Obamana atahitaji alitoe leo katika hotoba yake.
Mwandishi: Soric,Miodrag/ZR/Miraji,Othman
Mhariri:Abdul-Rahman