1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama atetea ushirikiano wa biashara na nchi za Pacific

Isaac Gamba
21 Novemba 2016

Rais wa Marekani Barack Obama ametetea ushirikiano wa biashara huria wa kiuchumi wa mataifa ya Asia na Pacific APEC

Peru APEC Gipfel Barack Obama Pressekonferenz in Lima
Picha: Picture-Alliance/dpa/Epa/E. Arias

Ushindi wa Donald Trump umeibua hofu juu ya kuwepo hatari ya kurejeshwa tena vikwazo vya kibiashara ambavyo ulimwengu umekuwa ukijitahidi kuviondoa, hasa baada ya bilionea huyo ambaye sasa atakuwa rais wa 45 wa Marekani kutangaza nia yake ya kuvunja mikataba kadhaa ya ushirikiano.

Ushindi wa Trump umegubika mkutano huo wa kilele wa ushirikiano wa kiuchumi wa nchi za Asia na Pacific, APEC, uliomalizika nchini Peru mwishoni mwa wiki, hali iliyopelekea  viongozi waliokuwa wakishiriki mkutano huo ikiwa ni pamoja na Rais Barack Obama, Xi Jinping wa China na Vladmir Putin wa Urusi kulazimika kufanya kazi ziada kutetea haja ya kuendelea kuimarishwa ushirikiano huo wa biashara huru.

Utandawazi na mikataba kadhaa ya kibiashara ni miongoni mwa masuala ambayo yamekuwa yakikosolewa  barani Ulaya na Marekani kwa ujumla kutokana na kile kinachoelezwa kutoa mwanya wa ajira zaidi kwa mataifa mengine na kusababisha hali duni ya maisha kwa baadhi ya raia, mambo ambayo yanaelezwa kuchangia zaidi katika ushindi wa Trump pamoja na hatua ya Uingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya - Brexit.

Katika mkutano huo wa APEC, hoja kubwa ilihusu mustakabali wa mkataba wa biashara huria kati ya Marekani na nchi za Pacific ujuilikanao kama TPP, ambao Marekani imekuwa ikiupigia upatu na ambao Rais Mteule wa Marekani Donald Trump aliahidi wakati wa kipindi chake cha kampeni kuufutilia mbali.

Rais Obama asisitiza ushirikiano huo kutovunjika

Rais Barack Obama na Rais Vladimir Putin wakijadiliana wakati wa mkutano wa APECPicha: picture alliance/Presidency of Peru

Hata hivyo, baada kumalizika kwa mkutano huo wa kilele hapo jana, Rais Obama alisema haitakuwa rahisi kuuvunja ushirikiano huo wa biashara huru kati ya Marekani na nchi za Pacific unaojumuisha nchi zipatazo 12 na kuwa nchi zilizoko ndani ya ushirikiano huo bado zina nia ya dhati ya kuendelea kushirikiana na Marekani.

Aidha Obama alisisitiza kwa wajumbe wa mkutano huo kuwa biashara inakuwa na mafanikio pale tu inapofanyika katika misingi inayokubalika na kuwa changamoto zilizopo zitatuliwa iwapo mafanikio yatokanayo na biashara hiyo yatawanufaisha  walio wengi zaidi na kuwataka  wale wenye mashaka na biashara huria katika kipindi hiki cha utandawazi kuzingatia misingi halali ya kibiashara na ndipo watakapopata manufaa ndani ya ushirikiano huo. 

Ama kwa upande mwingine Rais wa Urusi Vladimir Putin  alisema yeye na Rais Obama wamekiri kuwa na wakati mgumu katika mahusiano yao ya kikazi na licha ya hivyo wameendelea kuheshimiana  na kila mmoja kuheshimu msimamo wa mwenzie huku pia Rais Putin akimshukuru kwa ushirikiano aliotoa ktika kipindi chake chote cha uongozi na kumkaribisha wakati wowote atakapojisikia kutembelea Urusi.

Mwandishi: Isaac Gamba/AFPE

Mhariri: Mohammed Khelef